Sambaza....

1: Manchester United wameshanunua kifurushi cha kipindi cha pili. Waweza ukawatesa sana , ukawaonea na kuwabonda sana kipindi cha kwanza na kujiaminisha kuwa umewaweza. Na wakati mwingine ukawa na uhakika wa kushinda mechi hiyo, lakini ukweli unabaki pale pale, Manchester United imekuwa ikitoa tafasri halisi nini maana ya neno “mpira dakika 90”. Kipindi cha pili kila aina ya majini huwa upande wa Manchester United kuanzia mechi dhidi ya Newcastle mpaka mechi hii ya jana.

2: Chelsea iliwahi kuwa Didier Drogba, huyu walimtegemea sana, na yeye hakuwaangusha akawa anarudisha shukurani kwao kwa kufunga magoli. Alifunga sana, timu ikapata magoli sana na mwisho wa Siku akawa mfalme pale darajani. Hata wakati anaondoka wengi waliwaza sana, walijiandaa kuishi maisha magumu bila ya Didier Drogba, lakini kwa bahati nzuri walimpata Diego Costa. Huyu alikuwa na kiburi sana, mkorofi sana, mtukutu sana lakini alikuwa katili sana kwa magolikipa. Lakini alipoangusha kigombe cha kahawa cha Antonio Conte ikawa njia rasmi ya kuondoka pale Darajani. Tangu Siku hiyo Daraja halijawahi kuwa na mshambuliaji katili, na hiki ndicho ambacho mpaka sasa kimemsumbua jana Maurizio Sarri.

3: Alionekana kama ameanza kurudi sehemu ambayo maji hutokea. Sehemu ambayo wengi hutumia kukanyaga, baada ya yeye kukaa juu kwa misimu kadhaa hapa nyuma. Aliipa ubingwa Chelsea mara mbili, Jose Mourinho akaamua kumsogeza kama bidhaa hatari katika timu ambayo imawanajeshi hatari. Lakini msimu huu Nemanja Matic amekuwa mchezaji wa kawaida sana, lakini ukawaida ambao jana ameukataa na alikuwa nguzo ya matokeo ya jana.

4: Wakati Nemanja Matic akiwa nguzo katika mchezo wa jana, Antony Martial alizidi kumpa sababu kwanini Alexis Sanchez anastahili kukalia zile mbao. Mechi mbili magoli matatu, magoli ambayo yanazidi kumsogeza karibu na kiini cha mioyo ya mashabiki wengi wa Manchester United. Huyu ndiye mchezaji anayependwa zaidi na mashabiki wa Manchester United.Mashabiki ambao wanaamini anaweza kuibeba timu, na ndicho kitu ambacho amekifanya jana.

5: Manchester United imekuwa na matatizo ya sehemu ya ulinzi msimu huu lakini kuna tatizo ambalo kila siku wamekuwa wanakumbana nalo. Wamekuwa wakiruhusu sana magoli ya mipira iliyokufa. Hata goli la Antonio Rudigier lilikuwa kipimo sahihi cha makosa yao.


Sambaza....