Sambaza....

Licha ya kuwaacha Mashabiki wa Simba na wadau wa soka nchini katika hali ya furaha baada ya timu mbili za Tanzania kufuzu hatua ya nusu fainali katika michuano ya SportPesa lakini mchezo wa Mnyama Simba  dhidi ya AFC Leopard ya Kenya umeacha mambo matano ambayo kiukweli hakuna aliye yatarajia  kutokea, tena kwa kikosi kama cha Simba.

Mchezo wa Simba ulitanguliwa na mechi ya kwanza majira ya saa nane za mchana kati ya  Mbao FC na GorMahia ya Kenya ambaye ni bingwa mtetezi na Mbao kuibuka na ushindi kwa njia ya matuta na kufanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali.

Saa kumi  za jioni, mtanange wa Simba na AFC Leopard ulianza, na hadi dakika tisini zinamalizika Simba 2 AFC Leopard 1. Lakini mtanange huo uliacha vitu vipya vingi, ambavyo huenda vikazaa mfumo mpya ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Kwanza, mashabiki na wadau wa soka walikuwa na shauku ya kuwaona wachezaji wawili walioletwa kwa ajili ya kufanya majaribio katika kikosi cha Simba. Lamine Moro alianza katika nafasi ya ulinzi, akiwa bega kwa bega na Sergie Wawa, Moro alicheza dakika zote 90, ikiwa ni tofauti na mshambuliaji wa kigeni  Hunlede Kissimbo aliyecheza kwa dakika 45 pekee kabla ya kumpisha Meddie Kagere.


Hunlede Kissimbo , mchezaji anayefanya majaribio katika klabu ya Simba, naye akiwajibika katika mchezo wake wa kwanza na wekundu hao dhidi ya AFC Leopard.

wageni hawa walionyesha viwango tofauti huku Kissimbo akishindwa kuonyesha cheche zake katika mchezo huo wa kwanza kwa upande wake. kuna vitu vingi unaweza kuvieleza kutokana na kiwango chake lakini ni kawaida kwa mchezaji yeyote mgeni kuwa na kiwango kama kile kutokana na tofauti mza kimazingira na muunganiko na wachezaji wengine.

Naamini kocha wa Aussems atampa nafasi nyingi zaidi ili aweze kuonyesha kiwango halisi alichokuwa nacho. Kwa upande wa Moro, yeye alicheza katika nafasi ya beki wa kati, chini ya Paschal Wawa na baada Juuko Mursheed, kwa kiwango furani alionyesha kama ana uhai na kitu cha kuifanyia Simba japo kulikuwa na suala la uzito katika kuiondosha mipira na kufika maeneo husika kwa wakati sahihi na kuokoa mipira.

Jambo la pili, ni Rashid Juma kucheza nafasi ya ulinzi wa kushoto. Kiasili  Rashid Juma hutumiwa kama mshambuliaji wa pembeni yaani Winga, lakini katika mchezo huu alianzishwa katika eneo la ulinzi.

Maajabu aliyoyafanya ni kuitendea haki nafasi hiyo na kuonyesha kama yeye ni kiraka. Japo sio jambo geni kwa mshambuliaji wa pembeni kucheza katika nafasi ya ulinzi, kama ilivyokuwa kwa Nicholus Gyan ambaye nae alisajiliwa kama mshambuliaji wa pembeni lakini kwa sasa ndiye beki wa kulia tegemeo.

Rashidi Juma, kibelenge aliyechezeshwa katikaeneo la beki wa kushoto na kuonyesha maajabu yake katika mchezo wa Simba dhidi ya Leopard.

Rashid alifanikiwa hasa katika kulinda na kuanzisha mashambulizi, hakusita kubaki na mpira pale ilipohitajika kwa kuwa anajiamini na uwezo wake wa kupiga vyenga na hata kutembea na mpira, alikuwa na uwezo wa kumpunguza mchezaji mmoja hadi mwingine na kushambulia kwa kupitia pembeni, Simba ilipata faida katika eneo lake.

jambo pekee lililokuwa linamshinda ni kushambulia na kurudi kwa haraka katika eneo lake la ulinzi. Hii ilipelekea kuacha nafasi katika eneo lake na kukaribisha washambuliaji wa AFC Leopard kulitawala eneo lake na hata goli la Leopard lilitokea upande wa kulia.

Jambo la tatu ni Clatus Chama kupata kadi nyekundu. Si tukio la kawaida sana katika soka lakini limejitokeza katika mechi ya Simba na Leopard. Chama alizozana  na mwamuzi baada Mzamiru Yasin  kumfanyia rafu mchezaji wa Leopard, refa kwa kujichanganya alitoa kadi nyekundu kumzawadia Chama kisha akairudisha mfukoni na kumpa tena kadi ya njano. Wengi walicheka sana baada ya tukio hilo.

Tukio la nne ni Simba kuzidiwa umiliki wa mpira. Katika kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa sawa katika umiliki wa mpira yaani Simba ikimiliki mpira kwa asilimia 50 dhidi ya 50 za Leopard.

Haruna Niyonzima, kiungo wa Simba, akiwa katika harakati za kusogeza kabumbu mbele katika mchezo wao wa jana dhidi ya AFC Leopard.

Kipindi cha pili timu zote zilijitahidi kutengeneza nafasi za magoli, huku zote zikifungana goli moja. Lakini hadi dakika 90 zinakamilika Simba ilikuw na umiliki wa mpira kwa asilimia 48 dhidi ya 52 za Leopard.

Kwa upande wangu nilishangaa kidogo japo sio sana. Sababu kuu za kushangaa ni mazoea kutoka kwao, kwani kila mechi wanayocheza hasa mashindano ya ndani huwa wanamiliki mpira kwa asilimia kubwa kuliko timu pinzani, pili nilishangaa kwa kuona Chama na Haruna Niyonzima wakianzishwa wote na wakicheza kwa dakika zote 90 katika eneo la kiungo na timu bado inazidiwa umiliki wa mpira.

Tukio la tano ni kiwango cha beki wa kulia wa Simba, Zana Coulibaly. Zana ambaye alikuwa na kiwango hafifu katika mechi zilizopita kuanzia ligi kuu hadi mapinduzi ya Zanzibar alionesha kiwango kizuri kiasi cha watu kumuona ni beki mwenye msaada mkubwa katika timu.

Zana Coulibaly, akiwania mpira kutoka kwa mchezaji AFC Leopard katika mchezo wa kufuzu nusu fainali katika michuano ya SportPesa katika uwanja wa taifa, Dar es salaam.

Goli la kwanza ni pasi kutoka kwake baada ya kupiga krosi iliyomkuta Emmanuel Okwi katika eneo sahihi, na kufunga. Zana alijitahidi katika kuanzisha na kuzuia mashambulizi, alifanyiwa madhambi zaidi ya mara mbili, ame “clear” nafasi moja ya kufungwa akitokea pembeni kuokoa katikati baada  ya mabeki wa kati kupoteana.

Coulibaly amedhihirisha kuwa, ni suala la muda tu ndilo litakaloonyesha usahihi wa kiwango chake ndani ya wekundu wa Msimbazi. Tukumbuke kabla ya kusajiliwa, Coulibaly alikaa nje ya uwanja bila kucheza kwa kipindi cha miezi mitano. Kwa kiwango alichokionyesha ni dalili nzuri kuwa huenda akarudi katika kiwango chake alichokizoea.

Kwa upande wangu nakumbuka haya matano, bila shaka na wewe uliitazama mechi hii, ni tukio gani unalikumbuka, lililokuacha mdomo wazi?

Sambaza....