Beki wa pembeni wa timu ya soka ya Mwadui ya mjini Shinyanga Miraji Makka amesema imembidi kusafiri na timu kuelekea jijini Dar es Salaam ili kupambana na kuisaidia timu hiyo kusalia kwenye ligi kuu msimu ujao watakapocheza na KMC jioni ya leo kwenye uwanja wa Uhuru.
Makka ambaye amekuwa nje kwa muda sasa kutokana na majeraha amesema imebidi kusafiri kwani anatambua wazi kuwa Mwadui haipo sehemu salama kwenye msimamo na kama mwalimu atampanga licha ya kwamba bado anasikia maumivu atashuka uwanjani kupambana kuwania pointi tatu muhimu.
“Nimesafiri na timu licha ya kwamba bado ninasikia maumivu kwa mbali, unajua alama ambazo tunazo hazitoshi kabisa kusema kwamba tupo salama, bado tunahitaji kuondoka eneo hili na ndio maana nipo kwenye msafara huu, kama kocha atanipanga itanibidi nicheze ili kupambania timu yangu,” Makka amesema.
Beki huyo wa zamani wa Toto Africans na Stand United amesema anaamini kabisa kwamba Mwadui haitashuka daraja na imani hiyo inajengeka ukiangalia timu ambazo wamebakiza kucheza nazo na mechi ngumu pekee ni ambayo ipo mbele yao.
“Sasa tunakwenda kucheza na KMC ndo mechi ngumu ambayo mimi naiona, baada ya hapo tutaenda kucheza na Alliance na Mbao jijini Mwanza na baadae kumaliza na African Lyon na Ndanda, ukiangalia hapo hizo mechi nyingine sio ngumu kabisa kwa upande wetu,” amesema.
Mwadui wanashika nafasi ya 18 wakiwa na alama 37 baada ya kucheza na michezo 33, na wanahitaji wanalau alama 7 kujihakikishia kusalia kwenye ligi kwa msimu ujao.