SAID Juma Makapu aliingia uwanjani dakika za mwisho wakati Yanga SC ilipoendeleza ushindi wa asilimia 100 Jumapili iliyopita. Yanga ilishinda kwa mara ya nne mfululizo baada ya kuichapa Singida United 2-0 katika uwanja wa Taifa na Makapu aliingia dakika kumi za mwisho kuchukua nafasi ya Feisal Salum ‘Fei Toto.’
Feisal naweza kucheza Dar es Salaam-Pacha yake ya kwanza Jumapili hii dhidi ya mahasimu wao Simba SC lakini mchezo wake usio na nidhamu ya mchezo na ile ya kujiongoza humepelekea kupata kadi za njano tatu tena zile zisizo na faida kwa timu. Hadi sasa ni mchezaji anayetoa mchango mkubwa katika kikosi cha Mcongo, Zahera Mwinyi lakini kuelekea mchezo wa mahasimu , Makapu ni mchezaji anayehitajika mno kuliko Fei Toto.
Ndiyo, anaweza kuonekana anafanya vizuri kwa sasa lakini tatizo kubwa la Yanga ‘kukata pumzi’ dakika 15-20 za mwisho ni kiungo huyo wa timu ya Taifa ya Zanzibar. Akicheza eneo la chini-kiungo wa pili wa ulinzi mwenye jukumu la kuanzisha mashambulizi sahihi, Fei amekuwa akiwahi kuchoka na anapochoka kila kitu kizuri alichokifanya huanza kuwa kibaya.
Pasi zake nyingi zimekuwa zikipotea, na anapojaribu kuutafuta mpira mara nyingi hucheza faulo ambazo kimsingi si nzuri kwa timu yake kwa sababu hufanya karibu kabisa na eneo la hatari. Hata Makapu hucheza hivyo-mchezo wa kuchapa viatu, lakini nachokiona chenye faida kutoka kwake ni kwamba faulo zake ni za kitaalamu-huwaficha waamuzi na kupunguza kasi ya wapinzani.
Makapu tayari ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa kwa sasa, alicheza Dar-Pacha yake ya kwanza mwaka 2014 wakati huo Mbrazil, Marcio Maximo alipoamua kumuanzisha kikosi cha kwanza akiwa na miaka 19 mwezi Oktoba, 2014.
Alijitambulisha kama kiungo mlinzi mwenye mapafu ya kumuwezesha kuilinda ngome yake, huku stahili yake ya kucheza tackling zenye faida ikimfanya kuwa mmoja wa wakabaji wazuri katika soka la Tanzania. Feisal ni mkabaji ambaye anapenda kuuremba mpira pale anapoupata na ni wachezaji wachache sana waliokuwa na uwezo wa kukaba na kuuremba mpira mara baada ya kuupora-labda, Waziri Mahadhi ‘Mendieta’ ama Suleimani Matola ‘ Veron’
LAKINI wengi hasa kizazi cha sasa-mfano Himid Mao ni wakabaji ambao wakipora mpira jambo la kwanza ni kufikiria kuamisha –kuutoa eneo hatarishi na kuupeleka eneo salama. Makapu hana mambo mengi ndiyo maana mashabiki hawewizi kuona umuhimu wake, lakini kwa kocha anafahamu nini ambacho amekuwa akizalisha katika timu-kukaba vizuri na kuanzisha mashambulizi sahihi ya kushtukiza.
Ndiyo viungo wa kisasa walinzi wanavyofanikiwa, si kwa stahili ya Feisal-kupenda kuremba sana mpira na kucheza faulo za wazi ambazo katika michezo yake minne tu ya ligi kuu Tanzania Bara AMEPATA KADI TATU ZA NJANO, HUKU AKIWA MLALAMISHI MNO KWA WAAMUZI. Makapu ni mtu wa kupora mpira na kukimbiza mbele, hii ndio faida ambayo naiona inaweza kuisaidia Yanga dhidi ya Simba kutoka kwa Makapu.
Tayari ni mwenye uzoefu, anaweza kucheza katika eneo lake kwa muda wote wa mchezo, anaweza kupora mipira na kuanzisha mashambulizi, anaweza kucheza faulo za kitaalamu ambazo ni muhimu sana kwa timu katikati ya uwanja, anaweza kuzuia mpira unaopenyezwa njiani-hana kuremba mpira katika eneo lake hatarishi.
Zahera anajua wa kuwatumia, lakini ningemshauri kuitazama safu ya kiungo ya Simba, amtazame Makapu wa sasa nay ale yaliyozalisha katika Dar-Pacha, afanye maamuzi, si mengine ampe nafasi ya kuanza mchezo wa Jumapili, hakika hatamuangusha.