Watu wengi Ulimwenguni hupenda kusoma vitabu maarufu lakini watu makini Ulimwenguni hupenda kusoma vitabu bora pekee!
Jangwani pale (Yanga), kuna maktaba yenye vitabu vingi (Wachezaji), baadhi vimeshapotea na vingine vipo ila wasomaji wengi waliofika maktaba pale walisoma vitabu maarufu vingi kuliko vile bora!
Nazungumzia makocha wengi waliopita Yanga hawakuwa na imani juu ya ubora wa beki Said Juma Makapu kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ile ya kutozungumzwa saana na viongozi, hata magazeti lakini hawakujua.
Makapu yupo Yanga tangu mwaka 2014, akitokea Shangani fc ya huko zanzibar, bila shaka Yanga walimuona akiwa kwenye kikosi cha maboresho ya Taifa Stars mwaka huo akitumika kama kiungo mkabaji wakati mwingine beki wa kati na hata kulia.
Nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza Yanga siku za nyuma ilikua finyu sana, hatukumuona akicheza, hatukumuona kwenye benchi, lakini uwezo wake ulikua bado bora huko nje alikokua.
Ni Luc Eymael kocha Mbeligiji aliyezama maktaba ya Yanga na kukichukua kitabu hicho bora (Makapu) kilichokuwa kimepigwa vumbi kwa muda mrefu naye akaamua kukifuta na kukisoma kwa umakini.
Hakika umakini wa Luc katika chaguo la kitabu hicho (Makapu) kumempa maarifa makubwa ya kuilinda ngome ya Yanga dimbani.
Muda mchache tu tayari Makapu ametengeneza pacha iliyoimara na Lamine Moro, kamuweka nje mkongwe Yondani, amewafanya Wanajangwani kusahau kua wanaye Dante, Sonso na Ally Ally kwenye maktaba yao.
Kuna tofauti kati ya mashuhuri na mahiri, Makapu ni mlinzi mahiri, lakini kwakua Bongo kuna kasumba ya kuishi katika umashuhuri kuliko umahiri basi Makapu hazungumzwi katika ukubwa anaostahili.
Umri wa Makapu kwa mujibu wa pasi yake ya kusafiria “Passport” ana umri wa miaka 24, kwa maana hio Yanga na Taifa kwa ujumla wanayo kila sababu ya kumuamini zaidi na kumtunza kwani bado ana muda mrefu wa kutumika.