MPENDE mshambulizi huyu, lakini unaruhusiwa kutompenda. Kwa magoli yake saba katika michezo 12 ya ligi kuu Tanzania Bara aliyofanikiwa kuichezea Yanga SC, hakika mashabiki wa klabu yake wanajivunia kuwa na straika huyu lakini kwa wale wanaoangukia upande mwingine kiushabiki wanaweza kuendelea kumpinga lakini ukweli katika ligi ya msimu huu hadi sasa hakuna mfungaji mahiri kama Makambo.
GOLI LA KWANZA MCHEZO
Makambo tangu alipojiunga na Yanga katikati ya mwaka huu hajawahi kufunga magoli mawili au zaidi katika mchezo mmoja, lakini katika magoli yake yote saba aliyofunga kabla ya mchezo wa jioni ya leo vs Tanzania Prisons ni kwamba straika huyo mrefu amefunga goli la kwanza katika kila mchezo ambao alifunga.
Mechi yake ya kwanza tu ya ligi kuu Bara alifunga. Alifunga goli la kwanza katika ushindi wa 2-1 vs Mtibwa Sugar katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Akafunga goli pekee katika ushindi 1-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wake wa Tatu baada ya kushindwa kufunga katika ushindi wa 4-3 vs Stand United.
Goli vs Mtibwa alifunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael na lile vs Coastal pia alifunga kwa kichwa safari hii kwa msaada wa Ibrahim Ajib. Kocha Mcongo, Zahera Mwinyi alimuweka nje katika mchezo wan ne dhidi ya Singida United ili kumuacha ajiandae vizuri katika ‘Dar es Salaam-Pacha’ dhidi ya mahasimu wao Simba SC.
Hakukuwa na goli lolote katika game hiyo ya mahasmu Septemba 30. Makambo alicheza mchezo wa pili mfululizo pasipo kufunga wakati Yanga ilipoishinda Mbao FC 2-0 katika uwanja wa Taifa, lakini alirejea tena wakati alipofunga goli la uongozi vs Alliance School katika ushindi wa 3-0. Alifunga kwa kichwa na kwa mara nyingine ilikuwa ni kwa msaada wa Ajib.
Yanga ilisubiri hadi dakika ya mwisho kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya KMC FC katika mchezo wa mzunguko wa nane, shukrani kwa goli la mpira wa adhabu la kiungo Feisal Salum. Makambo akafunga goli pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Lipuli FC- safari hii kwa msaada wa Mrisho Ngassa.
Makambo hakufunga katika sare ya 1-1 dhidi Ndanda FC katika mchezo wa raundi ya kumi na wakati wengi wakitaraji kuona kipigo cha kwanza kwa ‘Timu ya Wananchi’ baada ya kuelekea Kanda ya Ziwa, Makambo akarahisisha kila kitu. Alifunga magoli ya uongozi ndani ya dakika 20 za kwanza vs Mwadui FC na Kagera Sugar FC katika viwanja vya Kambarage, Shinyanga na Kaitaba, Bukoba.
Yanga ilishinda 2-1, 2-1 dhidi ya timu hizo za Shinyanya na Kagera na aliporejea Dar es Salaam siku ya Alhamis iliyopita-kama ilivyo desturi yake, Makambo alianza kufunga goli la uongozi katika ushindi wa 3-0 dhidi ya JKT Tanzania. Kila alipofunga, Yanga ilishinda na si hivyo tu magoli yake yote saba ni yale ya uongozi ( magoli ya kwanza katika mchezop)
ANASTAHILI HESHIMA….
Mashabiki na wapenzi wa Yanga wanamuheshimu Makambo, wanampenda na wana mpa sapoti ya kutosha lakini kwa wale wanaoangukia mahala kwingine kiushabiki wao bado wanaona si mshambulizi wa daraja la juu.
Ni kumkosea heshima kwa maana kila mchezo aliofunga amefanya hivyo kwa ustadi mkubwa, pia isisahulike kuwa magoli yake yopte amefunga wakati matokeo yakiwa 0-0. Huyu ni mfungaji anayefunga wakati matokeo yakiwa 1-0, 2-0, 1u zaidi ya hivyo bali ni mfungaji bora wa goli la kwanza katika mechi na hakuna kama yeye.