Mchezaji anayeitwa Yannick Bangala anapitia kipindi kigumu hivi sasa pale Jangwani.
Haieleweki kama msimu ujao atakuwa mchezaji wa Yanga SC au laa. Kiufupi yuko kizani.
Jana hakuwa sehemu ya utambulisho wa wachezaji wa Yanga SC msimu ujao. Isingetarajiwa kuwa mapema kwa kiasi hiki.
Maisha yamemuwendea kasi. Miezi 12 iliyopita ni yeye aliyekuwa MVP wa ligi yetu. Mechi nyingi za Yanga SC walicheza katika mdundo wake. Ni yeye aliyekuwa anaamuru timu icheze katika mdundo upi.
Lakini leo vitu vingi viko tofauti kwa upande wake. Mwishoni mwa msimu uliopita tayari alishapoteza nafasi yake kiwanjani.
Kupoteza nafasi ni kama ilianza kupoteza umuhimu wake ndani ya timu. Nadhani yuko njia ya panda ya soka lake.
Huenda akabakia Yanga SC, akaenda timu nyingine au akarudi kwao. Vyote vinaweza kumtokea, lakini kuhamia timu nyingine na au kurudi kwao ni kitu ninachokitarajia.
Lakini kuna kitu kimenishangaza hapa kwa Bangala. Imekuwaje mchezaji mahiri aliyetoka kushinda MVP miezi 12 iliyopita, ghafla anaonekana kachuja? Ni swali gumu.
Wachezaji huwa wanapita katika mchakato mpaka wanafikia kuonekana wa kawaida kabisa. Haiwi haraka haraka kama ilivyomtokea Bangala.
Nilitegemea Bangala angeendelea kusukuma siku pale Jangwani na kupungua makali yake kidogo kidogo, mpaka baadae kila mmoja kusema amechuja.
Lakini kwake haiko hivyo. Ameporomoka ghafla. Sijui kama mwenyewe analijua hili. Mwisho wa siku Yanga SC watampa mkono wa kwaheri. Tujiandae na maneno mawili ya “THANK YOU.”
Sjui nini kitokee ili Bangala awe sehemu ya Yanga SC msimu ujao. Klabu za mpira zinaendeshwa Kibepari, sio kijamaa.