Haikua rahisi wala kitu ambacho Wananchi Yanga walikitaka kuachana na kocha wao kipenzi Nasraddine Nabi ambae rasmi jana wameachana nae na kumtakia kila lakheri, lakini wakakiri mafanikio ya Yanga hayakuletwa na Nabi pekeakee.
Nabi amedumu Yanga kwa misimu miwili na nusu huku akichukua ubingwa mara mbili wa Ligi na mara moja akichukua bila kupoteza huku pia akiifikisha fainali ya kombe la shirikisho.
Kufuatia kuondoka kwake baadhi ya nyota wa Yanga wamemuaga nyota huyo huku wakiwa na maneno mengi ya kusema kwa Mtunisia huyo. Makamu mwenyekiti wa zamani wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema “Kiukweli Nabi ametufanyia mambo makubwa sana Yanga lakini mafanikio ya Yanga yamechangiwa na vitu vingine zaidi pia kama uongozi bora.”
Nae mlinzi wa kulia Kibwana Shomari aliandika hivi katika ukurasa wake “Ulikuwa sio mwalimu tu ila kama mzazi na rafiki wa kunifanya niwe imara na kunipa matumaini na kunifundisha kwenye kila hatua niliyo piga kuelekea kutimiza ndoto zangu.”
Pia nyota aneuhusishwa kuondoka pia dirisha hili la usajili Fiston Mayele amemtakia kila lakheri Nabi akisema ameifanyia kila kitu Yanga “Kila la kheri kocha, ulifanya kila kitu kwa Yanga,” alisema Mayele.
Nae beki bora wa msimu huu wa ligi ya NBC Dickson Job aliandika “Ulikua kama mwalimu, baba, rafiki, siku zote nilijua kucheza lakini ulinifundisha namna ya kushinda. Daima utabaki kuwa kocha wangu na sitoweza kushukuru kiasi cha kutosha kwa mema yote uliyonifanyia. Kwaheri ya kuonana Baba Nabi.”
Mfungaji wa bao pekee katika mchezo wa fainali ya FA Kennedy Musonda amesema “Asante Profesa kwa kila kitu ulichofanya kwangu kwa miezi michache. Umenifundisha kuhusu mchezo na umenisaidia kuwa mchezaji mzuri zaidi.”