Sambaza....

Jana Jurgen Klopp alifanikiwa kuvunja utawala wa Manchester City wa kwenda mechi mechi 22 bila kufungwa.

Anazidi kujiwekea rekodi nzuri dhidi ya Pep Guardiola, mpaka sasa katika michezo 12 waliyokutana Jurgen Klopp kafanikiwa kushinda michezo 6 na kutoka sare mchezo mmoja huku Pep Guardiola akishinda mechi 5.

Jana Manchester City walicheza mfumo wa 4-3-3, wakati Liverpool pia walitumia mfumo wa 4-3-3 baada ya kupata goli walibadirika na kuanza kutumia mfumo wa 4-5-1.

Kumwanzisha Andrew Robertson upande wa beki wa kushoto dhidi ya timu ambayo wachezaji wake wa pembeni wamehusika kwenye magoli kwa kiasi kikubwa ilikuwa kama kamari.

Mchezaji ambaye alikuwa na michezo nane (8) kabla ya mchezo wa jana akapambane na Raheem Sterling ilikuwa ni kuinamisha kichwa na kujidai kutokuona kinachotokea.

Lakini Andrew Robertson alifanikiwa kumzuia Raheem Sterling na hii ni kutokana na sababu kuu moja.

Mabeki wote wa pembeni wa Liverpool ( Gomez na Robertson ) walikuwa wanapanda kwa tahadhari mbele kwenda kusaidia mashambulizi.

Asilimia kubwa ya muda wao waliutumia nyuma kuwakaba Sane na Sterling hali ambayo iliwanyima uhuru kwa kiasi kikubwa.

Ilikuwa ni mara chache kwa Lovren na Matip kuonekana wakienda kusaidia upande wa kushoto au kulia kwa sababu muda mwingi Robertson na Gomez walikuwepo kule.

Hali ambayo iliwafanya pia kina Matip na Lovren kusimama eneo moja , eneo ambalo walisimama na Sergio Aguero kwa muda wote.

Kwa kiwango cha jana cha Sergio Aguero kimeonesha kwanini Alexie Sanchez anahitajika katika kikosi cha Manchester City.

Kwa sababu, jana Sergio Aguero muda mwingi alitumia kukaa eneo moja. Kitu ambacho kilikuwa rahisi kwa mabeki wa kati wa Liverpool kuendana nacho.

Hakuwa na mijongeo au kasi ambayo ingewalazimu mabeki wa kati wa Liverpool kufanya makosa binafsi.

Pia hakuna uwazi uliotengenezwa sehemu ya nyuma ya Liverpool ili kuweza kuwasaidia kina Kelvin De Bryune, Gundogan kuutumia wakitokea katikati, kwa sababu ya Aguero kutumia muda mwingi akiwa eneo moja bila kuhama.

Kuna wakati Pep Guardiola alimtaka Van Djik na John Evans. Jana kumedhihirisha kwanini Pep Guardiola anahitaji beki wa kati.

Manchester City kabla ya mechi ya jana ndiyo ilikuwa timu ambayo imefungwa goli chache, hii kwa tafasri ya haraka haraka ni kwamba Manchester City walikuwa na safu imara ya ulinzi. Kitu ambacho kiuhalisia siyo kweli kwa sababu Manchester City hujilinda kwa kumiliki mpira kwa muda wote.

Jana mabeki wake wa kati walikuwa siyo wepesi kufanya maamuzi, mfano goli la Roberto Firmino, John Stones alichelewa kufanya maamuzi kuuondoa ule mpira.

Pia makosa mengi binafsi yalionekana kati yao wawili ( Otamendi na John Stones).

Ukiachana na mabeki wa kati, Manchester City hawana mtu sahihi wa kukaa eneo la Mendy. Danilo alisajiliwa kwa ajili ya kubadilishana na Mendy, lakini jana alipoingia kuchukua nafasi ya Fabian Delph hakuwa na uwezo mzuri kipindi timu ilipokuwa inakaba na kipindi timu ilipokuwa inashambulia.

Oxlaide Chamberlaine kumwanzisha eneo la katikati la uwanja kushoto lilikuwa na msaada mkubwa kwa Liverpool kwa sababu Liverpool ilikuwa inaanza kushambulia kwa kasi kuanzia eneo la katikati uwanja.

Hali hii ilikuwa inawapa nafasi Liverpool kuwa na watu wanne wenye kasi kule mbele ( Mohammed Salah, Roberto Firmino , Saido Mane na Oxlaide Chamberlain aliyekuwa anatokea katikati kuja mbele).

Wote walikuwa wanakabia juu, hali iliyowafanya Manchester City kufanya makosa binafsi.

Kila walipokuwa wanakabia juu kwa kasi walikuwa wanafanikiwa kupata mipira na kuanzisha mashambulizi kwa kasi.

Liverpool walijua Manchester City huanza kutengeneza mashambulizi yao nyuma, ambapo mabeki hushuka mpaka katikati ya uwanja ili kuisukuma timu iwe mbele na mpinzani awe nyuma.

Hivo Liverpool walichokifanya ni wao kuanzia kukabia juu ili kuwafanya mabeki wa Manchester City wafanye makosa binafsi.

Ukiangalia magoli ya Firmino, Sane na Salah. Yalianza wakati ambao Manchester City wakiwa wanaanza kutengeneza mashambulizi nyuma, hivo Liverpool kufanikiwa kukawakabia juu na kuanzisha mashambulizi kwa kasi kabla safu ya ulinzi ya Liverpool haijajipanga vizuri na kufanikiwa kufunga magoli.

Sambaza....