Sambaza....

Abdul Mohamed alikuwa na maono, maono ambayo yalikuwa ni msingi wa kuiimarisha Azam FC na kuwa timu imara kwa muda mrefu

Aliamini katika karatasi zake alizotumia kuandika maono yake, usingizi ulikuwa siyo rafiki kwake bila kusoma karatasi za maono yake.

Karatasi ambazo zilikuwa na njia ambayo ilikuwa inamuonesha ni wapi anatakiwa kupitia ili kufika anapopatamani.

Matamanio yake yalikuwa kuiona Azam FC ikitegemea vijana kwa asilimia kubwa vijana ambao klabu ilikuwa inatumia gharama kubwa kuwaibua, kuwalea katika kituo chao.

Aliona ni wakati sahihi kwake yeye kuona kituo chao cha vijana kikiinufaisha timu kubwa.

Macho yake yaliona taswira ya “La Masia” kila mguu wake ulipokuwa unakanyaga Azam Complex.

Nguvu ya matamanio yake iliongezeka maradufu moyoni mwake.

Abdul Mohamed

Kitu kilichompelekea kuchukua maamuzi, maamuzi ambayo wengi waliona ni maamuzi ambayo yangesababisha Azam FC kufanya vibaya.

Nyota wake waliondoka, nyota ambao walionekana kama ni wachezaji muhimu katika kikosi cha Azam FC.

Lilikuwa jambo la kushangaza kwa sababu kama lengo kubwa la Azam FC ni kuwa na timu imara ilikuwaje wao wakawaruhusu wachezaji imara kuondoka?

Golikipa bora wa ligi kuu Tanzania kwa mara mbili mfululizo (2015/2016 na 2016/2017) alikuwa mikononi mwao lakini hawakuogopa kuiruhusu mikono yao imwachie tena kwa watu ambao ni wapinzani wake kwenye mbio za ubingwa.

Aishi Manula akapishana na Razack Abalora, lango la msimbazi likawa mikonono mwa Aishi Manula na lango la Chamazi likawa mikononi mwa Razack Abalora.

Hapana shaka Razack Abalora amewasahulisha Azam Fc kuhusu Aishi Manula.

Kusahau kwao hakumanishi kuwa Aishi Manula anafanya vibaya Simba, ni moja ya nguzo imara kati ya nguzo zinazosimamisha ghorofa la msimbazi

Michezo 12 bila kufungwa goli lolote katika michezo 19 ni jambo ambalo linadhihirisha mikono yake ni imara kama ilivyokuwa Chamazi.

Mikono ambayo inahakikisha ulinzi dhabiti wa magoli ya John Bocco, nyota ambaye alishiriki kuipandisha timu ya Azam FC 2005 na kuwa nayo mpaka mwaka 2017

Miaka takribani kumi na mbili (12) jasho lake likitoka kwa kuipigania Azam FC katika majira ya joto na baridi.

Nyakati ngumu na nyakati za furaha alikuwa pamoja nao, aligeuka kuwa kipenzi cha wachezaji wenzake kwa sababu ya busara ambayo ilikuwa inahubiriwa kuwa anayo.

Uwezo wake wa kuwaongoza wachezaji wenzake , kuwaweka pamoja na kupigana kwa ajili ya timu bila kukata tamaa ilikuwa sifa yake ya ziada baada ya ile sifa ya kupachika mabao.

Mabao yake yalionekana hayana muhimu tena katika kikosi cha Azam FC, klabu haikumpa heshima yake stahiki, pamoja na kucheza pale kwa miaka takribani 12 timu ilimwacha kama mtu ambaye hakuwa na mchango mkubwa pale Azam FC.

Waliyafagia magoli, Simba wakayaokota na kuyatumia na ikizingatia walikuwa na njaa hawakuona ajizi kuyatumia ili kukidhi shibe yao.

Magoli 10 mpaka sasa akiwa nyuma ya Chirwa mwenye magoli 11 na Okwi mwenye magoli 16

Magoli yake yamekuwa msaada mkubwa kwa Simba mpaka muda huu.

Hutakiwi kushangaa namna ambavyo Erasto Nyoni anavyokuwa anajitahidi kuyalinda magoli ya John Bocco tena katika namba tofauti. Mpaka sasa ndiye mchezaji pekee kwenye ligi kuu msimu huu aliyecheza nafasi nyingi ndani ya uwanja.

Amecheza kama kiungo wa kati wa eneo la kuzuia, beki wa kulia , beki wa kushoto na beki wa katikati. Nafasi nne tofauti ndani ya msimu mmoja !, nafasi ambazo zimemsaidia kutoa pasi sita (6) za mwisho za magoli mpaka sasa achana na magoli ambayo amefunga na kuisaidia timu.

Shomari Kapombe

Azam FC hawakuogopa kumuacha kwa sababu lengo lao lilikuwa kuingiza damu changa kwenye timu kubwa, ikawa jambo la kawaida kwao kumwacha hata Shomari Kapombe ambaye aligharamikiwa vizuri na Azam FC kipindi yuko na majeraha.

Gharama za matibabu zilikuwa chini ya Azam FC tena kwenye hospitali za hadhi ya juu nchini Afrika Kusini, lakini mwisho wa siku akaenda Simba.

Hii ilikuwa lazima yeye aende Simba kwa sababu Azam FC walitaka kutoa mabati ambayo yalionekana makuukuu kwao na kuezeka mabati mapya.

Ukuukuu wa mabati haya kwa Azam FC hayakuonekana kwa Simba, hawakuona aibu kuyabeba na kwenda kuuzeka kwenye nyumba yao kitu ambacho kimesaidia paa la nyumba yao kunawiri na kuvutia machoni.

Sambaza....