Uongozi wa klabu ya soka ya Lipuli ‘Wanapaluhengo’ umekanusha taarifa za kupokea maombi kutoka katika klabu ya Dar Young Africans ya kutaka kumsajili mshambuliaji wao kinda Adam Salamba.
Lipuli kupitia kwa Msemaji wao Clement Sanga wameiambia Kandanda.co.tz kuwa huo ni uvumi wa mitandao ya kijamii na kwamba Salamba bado ni mchezaji wao halali na bado yupo katika mipango ya klabu kuelekea katika michezo ya mwisho ya ligi kuu ya kandanda Tanzania Bara.
“Kumekuwa na taarifa kuhusiana na mshambuliaji wetu Adam Salamba, na leo tena kupitia mitandao ya kijamii kumeibuka habari ya kwamba anawaniwa na Yanga kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya michuano ya kombe la Shirikisho Afrika,”
“Lakini mpaka naondoka ofisini, hatujapokea barua yoyote ya kiofisi kutoka Yanga kuhusiana na kumuhitaji mchezaji huo, lakini Adam bado yupo katika mipango yeu, tunahitaji sana kumtumia msimu huu na msimu ujao pia,” amesema Sanga.
Kwanini Salamba
Saramba ambaye alianza kuonekana msimu uliopita akiwa na klabu ya Stand United amekuwa gumzo kwa siku za hivi karibu kutokana na kuonesha kiwango mujarabu katika mechi za ligi kuu.
Hali iliyofanya bodi ya ligi kumchagua kama mchezaji bora wa ligi kuu katika mwezi wa tatu, na amekuwa akitajwa sana kuwapo katika mipango ya timu ya soka ya Yanga ambayo imekuwa ikihitaji sana mshambuliaji wa kariba yake.