Katika sherehe za ugawaji tuzo za FIFA zilizofanyika Paris Ufaransa taifa la Argentina limeibuka kinara katika kubeba tuzo hizo huku mafanikio yao yakubeba Kombe la Dunia yakichagiza kwa kiasi kikubwa.
Mshambuliaji wa Argentina na Paris St-Germain Lionel Messi amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka kwenye Tuzo za Fifa za 2022 kwa upande wa wanaume.
Lionel Messi mwenye umri wa miaka 35 aliwashinda washambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe na Karim Benzema waliongia katika tatu bora ya mwisho.
Baada ya kutwaa tuzo hiyo Messi alisema “Nilifanikisha ndoto niliyokuwa nikitarajia kwa muda mrefu. Watu wachache sana wanaweza kufikia hilo na nimekuwa na bahati kufanya hivyo.”
Pia kocha Lionel Scaloni, ambaye aliiongoza Argentina kutwaa taji lao la tatu la Kombe la Dunia, alitawazwa kuwa kocha bora wa mwaka wa wanaume mbele ya Pep Guardiola wa Machester City na Carlo Anchelotti wa Real Madrid.
Kwa upande wa wanawake Alexia Putellas wa Barcelona alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka na goli bora Kwa upande wa tuzo ya “Puskas” goli bora la mwaka imekwenda kwa Marcin Oleksy.
Kocha wa England, Sarina Wiegman alitawazwa kuwa kocha bora wa mwaka wa wanawake baada ya kukiongoza kikosi cha England kutwaa ubingwa wa Ulaya nyumbani mwaka jana, likiwa ni taji la kwanza kuu kwa timu hiyo.
Mlinda mlango wa Aston Villa na Argentina Emiliano Martinez alitangazwa kuwa mlinda mlango bora kwa wanaume, huku Muingereza Mary Earps akishinda tuzo ya wanawake.
Martinez, 30, aliisaidia nchi yake kushinda Kombe la Dunia, akiokoa penalti muhimu katika michezo ya nusu fainali na fainali dhidi ya Ufaransa.
Earps, anayechezea Manchester United katika Ligi Kuu ya Wanawake, alianza mechi zote sita za England kwenye Euro 2022 huku wakishinda michuano hiyo.