USHINDI wa 2-0 ambao timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) imeupata jana Jumanne dhidi ya Cape Verde Islands umefufua matumaini ya Stars kufuzu kwa fainali za kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Cameroon hapo mwakani.
Stars imefika alama tano katika kundi L na kukamata nafasi ya pili mbele ya Cape Verde wenye pointi nne na Lesotho wenye alama mbili huku vinara Uganda wakihitaji walau pointi moja tu kufuzu kwa mara ya pili mfululizo fainali hizo kubwa zaidi za soka barani Afrika.
MAMBO BADO…
Kuifunga Cape Verde ni mtaji mkubwa, lakini ili kufuzu kwa fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri miaka 38, Stars inatakiwa kukaza mkanda. Kimahesabu-Uganda wanahitaji alama walau moja ili kwenda Cameroon na mchezo wao ujao watawakaribisha Cape Verde ambao kimsingi wanaweza kufikisha alama kumi endapo watashinda dhidi ya Uganda ( ugenini) kisha Lesotho ( nyumbani)
Sare Kampala inaweza kufufua matumaini ya Cape Verde na huenda wakafuzu endapo Stars itapoteza Lesotho katika mchezo ujao. Kama Cape Verde itafanikiwa kupata walau alama moja na Stars kupoteza inamaanisha visiwa hivyo vya Kaskazini Magharibi mwa Afrika vitakuwa juu ya Stars kutokana na matokeo ya –head to head.
Kupoteza dhidi ya Lesotho kutaifanya nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika kuwa juu ya Stars kutokana na matokeo ya wenyewe kwa wenyewe hivyo kwa namna yoyote ile Tanzania inapaswa kujizatiti na njia mojawapo ya kuweza kuweka hai matumaini ya kwenda Cameroon ni kutopoteza dhidi ya Lesotho.
Ukitazama katika kundi, Lesotho ni wapinzani wetu wa karibu mno licha ya kwamba kwa sasa wapo nyuma ya Stars kwa alama tatu. Kama timu zikilingana pointi – Caf hutumia kwanza kigezo cha kutazama matokeo ya head to head hivyo kwa mpango huo unaweza kuona ni kiasi gani bado kikosi cha Mnigeria Emmanuel Amunike kina kazi kubwa ya kufanya.
Huwezi kuwatoa Cape Verde wala Lesotho katika kuwania nafasi ya pili ambayo kimsingi ndiyo inaweza kuifanya Stars kufuzu kwa fainali za mwakani. Kama tutalingana alama na Cape Cerde inamaanisha watakuwa juu yetu kutokana na matokeo ya 3-0, 2-0 yaliyotokea katika michezo miwili iliyopita.
Pia endapo tutapoteza dhidi ya Lesotho- pia tutakuwa nyuma yao kutokana na kwamba mchezo wa kwanza ulimalizika kwa sare ya kufungana 1-1 Dar es Salaam. Hivyo, huu si wakati wa kuanza kuamini moja kwa moja kuwa nafasi ya kufuzu CAN kwa mara ya pili tangu mwaka 1980 bado haiwezi kupatikana kutokana na matokeo ya jana tu.
Kupata alama walau moja dhidi ya Lesotho inaaminisha tutaiondoa kabisa nchi hiyo katika mbio za kufuzu, lakini kupoteza ama matokeo ya sare ni jambo ambalo litazima kila ndoto za Watanzania hivyo ieleweke bado kuna ushindani mkubwa katika ya Tanzania, Cape Verde na Lesotho katika kuwania nafasi moja iliyosalia katika kundi baada ya Uganda kuomnekana ‘wata-hodhi’ nafasi ya kwanza.