KUFUNGA magoli 23 katika msimu wake wa kwanza wa ligi kuu Tanzania Bara, kufunga magoli sita katika michezo 12 ya ligi ya mabingwa, magoli mengine manne katika klabu bingwa Afrika Mashartiki na Kati- Kagame Cup, goli moja moja katika michuano isiyo rasmi ya Mapinduzi Cup na SportPesa Super Cup bado hakukutosha kumpatia tuzo ya mshambuliaji bora wa klabu yake Mnyarwanda, Meddie Kagere.
Klabu ya Simba SC iliwatunikia wachezaji wake tuzo mbalimbali usiku uliopita ikiwa ni muendelezo wa tuzo hizo zilizoanza kutolewa msimu uliopita chini ya mwekezaji mkuu wa klabu hiyo-tajiri, Mohamed Dewji ‘MO’.
Katika tuzo hizo tulishuhudia nyanda Aishi Manula akitetea tuzo yake ya golikipa bora wa klabu dhidi ya aliyekuwa mshindani mwenzake, Deogratius Munish ‘Dida’, Erasto Nyoni alitwaa tuzo ya mchezaji bora-chaguo la wachezaji wenzake na ile ya beki bora, Mghana, James Kotei alishinda tuzo ya mchezaji bora wa nafasi ya kiungo, wakati nahodha wa kikosi hicho, John Bocco yeye alishinda tuzo ya mshambulizi bora wa mwaka wa klabu, na Kagere akatwaa tuzoya mchezaji bora wa mwaka wa klabu.
KAGERE……
Kushindwa kwake kutwaa tuzo ya mshambuliaji bora wa mwaka na kushinda ile ya mchezaji bora wa mwaka kwa kiasi Fulani inashangaza, na nadhani mshambulizi huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda alistahili kushinda tuzo zote hizo licha ya ukweli pia Bocco alijitoa sana na kufanya mambo makubwa msimu uliopita.
Mafanikio ya kwanza kwa mshambulizi yoyote ni kufunga magoli na katika hilo, Meddie alikuwa bora kwa msimu mzima ndani na hata katika michuano ya Caf ambayo magoli yake yaliisaidia Simba kufika hatua ya nane bora kwa mara ya kwamba tangu mwaka 2003.
Bocco amemaliza msimu akiwa nyuma kwa magoli saba dhidi ya Kagere katika ligi kuu pekee, na huku akifunga magoli mawili tu katika michuano ya Caf huku akishindwa kufunga goli lololte katika hatua ya makundi ni wazi amekuwa na bahati kwa ‘kupewa’ tuzo hiyo ambayo pia alishinda msimu uliopita.
…uchambuzi unaendelea baada ya takwimu hizi.
Kama mshambulizi hupimwa kwa wastani wake wa kufunga, Meddie ni bora Zaidi ya wote klabuni Simba msimu uliopita na Mnyarwanda huyo kwa hakika alistahili kushinda walau tuzo mbili usiku wa Mo Awards-tuzo ya mshambulizi bora na ile ya uchezaji bora wa mwaka klabuni kwake. Samba haikuwa timu bora sana uwanjani, lakini Kagere alikuwa bora mno na mshambulizi huyo ‘amepunjwa’ kile alichostahili kushinda kutokana na kazi yake.
Kiujumla licha ya ‘sintofahamu’ kadhaa kuhusu washindi kama, Erasto ambaye alishinda tuzo ya mchezaji bora-mlinzi mbele ya Muivory Coast, Paschal Wawa, na ile ya Bocco tuzo hizo zilifana na zilivutia. Ni kwanini Bocco na si Kagere kama mshambulizi bora wa msimu Simba ?