Sambaza....

Ilikuwa siku ya tarehe 14 Mei 2014 baada ya pilika za kutwa nzima, mimi na genge langu tumejikusanya ndani ya AD Pub mjini Sinza kushuhudia mtanange wa fainali ya Europa League kati ya Sevilla na Benfica.

Hii ilikuwa ni fainali ya pili mfululizo kwa Benfica baada ya kupoteza fainali ya msimu uliopita kwa goli 2-1 dhidi ya Chelsea. Wadau karibia wote tulikuwa upande wa Benfica ikiongozwa na kiungo mtaalam wa boli Oscar Cardozo.

Mechi ilikuwa kali sana, bila shaka ndugu yangu Gerald mwana wa Lyanda ambaye kwa sasa yupo Chunya Makongolosi anaikumbuka hii mechi vizuri. Benfica walishambulia sana, walikosa magoli sana ndani ya dakika 120. Mwishowe mechi ikabidi iamriwe kwa mikwaju ya penalty. Benfica ikapoteza tena, mimi na wadau wangu pia tukaangukia pua kwa mara ya pili.

Hii ilikuwa ni fainali yao ya nane katika michuano ya ulaya tangu 1962 na hawajawahi kushinda hata moja.

Benfica ikiwa chini ya kocha Bela Guttman ilikuwa ni tishio na yenye mafanikio makubwa. Aliiwezesha kuchukua kombe la klabu bingwa Ulaya mara mbili mfululizo mwaka 1961 na 1962.

Bella Guttiman.

Kutokana na mafanikio hayo Guttman aliuomba uongozi wa Benfica umuongezee mshahara. Wajomba wakamuona mpuuzi wakakataa kumuongeza. Guttman alikasirika sana na kusema kuwa, Benfica haitakuja kuchukua ubingwa wowote wa Ulaya mpaka ipite miaka 100. Kwa maana hiyo ikiwa huu ni mwaka 2022 bado kuna miaka 40 ya msoto kwa Benfica ndio waanze kushinda mataji ya Ulaya.


Sambaza....