Sambaza....

Jana timu ya taifa ya Tanzania ilikuwa uwanjani kutafuta alama tatu ambazo zingeiwezesha kufuzu moja kwa moja kwenye michuano ya Afcon lakini kwa bahati mbaya walifungwa goli moja kwa bila na kuwalazimu kusubiri mpaka mechi ya mwisho ambayo itaamua nani atakayeweza kufuzu.

Hizi hapa ni sababu ambazo zilisababisha Taifa Stars kufungwa katika mechi ya Jana.

1: Ukosefu wa nidhamu ya kimaamuzi kwa wachezaji wa Taifa Stars.


Mechi ya jana ilikuwa mechi ambayo ilikuwa na presha kubwa ndani yetu. Mashabiki walikuwa wanatamani kuiona timu ikifuzu kwenda Cameron.

Viongozi wa serikali walikuwa na shauku ya kuiona timu yao ya Taifa ikishinda mechi hii. Kitu ambacho kiliongeza presha ndani ya wachezaji wetu.

Wachezaji wetu walikuwa na presha kubwa kila wakikumbuka watu ambao walikuwa nyuma yao. Na inavyoonekana hawakuandaliwa kuipokea presha ile.

Msimamo wa kundi L (Livescore)

Kitu hiki kilisababisha wachezaji wengi kutokuwa makini katika maamuzi yao ndani ya uwanja. Wengi walikuwa wanapoteza mipira, hata kona iliyosababisha goli ilitokana na mabeki kukosa maamuzi mazuri ya kuutoa huo mpira baada ya kukosa mawasiliano mazuri. Presha hii kubwa ilisababisha tushambuliwe kwa muda mrefu.Hatuna wachezaji ambao wanaweza kucheza kwenye presha kubwa.

2: Uchaguzi wa wachezaji katika kikosi cha kwanza.


Lengo la mwalimu Emmanuel Amunike kuanzisha wachezaji nane wenye asili ya kuzuia lilikuwa kuifanya timu icheze kwa kujilinda na isiruhusu goli na sisi tupate goli hasa hasa dakika za mwanzo.

Ndiyo maana dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza na kipindi cha pili tulikuwa tunafanya mashambulizi ya kupata goli la mapema ili tujilinde kitu ambacho hakikufanikiwa.

Kosa kubwa ambalo tulilifanya ni kuwachezesha wachezaji katika eneo ambalo siyo lao. Mfano kumchezesha Gadiel Michael kama winga na mabeki kama Abdalah Kheri kuwa beki wa pembeni wakati kihalisia ni beki wa kati.

Hii ilisababisha wachezaji hawa kutomudu nafasi zao, na mashambulizi mengi ambayo tulikuwa tunashambuliwa yalikuwa yanatokea katika eneo la pembeni kushoto na kulia.

3: Ukosefu wa Mbwana Ally Samatta.


Jana kabla ya mechi niliandika kitu kimoja kubwa, Mbwana Samatta amekuwa nguzo muhimu ya magoli yetu kwa sababu mpaka sasa tumefunga magoli 3 na yote Mbwana Ally Samatta kahusika kwa 100%.

Jana hakuwepo, kitu ambacho kiliharibu umbo zima la timu kule mbele na kumsababisha Simon Msuva kuwa nje ya eneo lake Mara kwa Mara na hakukuwepo na uelewano mzuri kati yake na Shaban Chilunda, ingawa Chilunda alicheza vizuri .

4:Kukosekana kwa Kiungo wa kati mwenye asili ya ushambuliaji.

Jana walicheza viungo ambao wana asili ya kuzuia. Kipindi cha kwanza mwanzoni , Himid Mao na Mudathir Yahaya walicheza eneo la kati kabla ya Himid Mao kwenda pembeni kulia na Erasto Nyoni kuja kucheza katika eneo la kiungo cha kati.

Hawa wote wana asili ya kukaba. Kitu hiki kilikuwa kinasababisha uwazi kuanzia eneo la kiungo wa kati wa kushambulia na eneo la ushambuliaji.

Kuna wakati Simon Msuva alikuwa anashuka chini katikati kufuata mipira, na hii ni kwa sababu alikuwa hapati huduma ya mipira , kitu ambacho kilimlazimu yeye kuwa anashuka kuichukua hiyo mipira.

Sambaza....