Mimi na wewe huenda tunasikia tetesi kuwa Benard Morrison amemwaga wino ndani ya Simba lakini tusiwe na ukweli wa moja kwa moja. Hata kama jambo hili ni kweli basi litabaki kuwa siri kutokana na kanuni za usajili wa ligi yetu kwa maana klabu yoyote hairusiwi kufanya mazungumzo na mchezaji yeyote ambaye bado hajamaliza mkataba na klabu nyingine.
Habari hii iliwekwa tarehe 07/07/2020 na leo tarehe 08/08/2020 yametimia, soma zaidi kwanini leo hii imekuwa kamili.
Kanuni hii imeahidi kutoa adhabu kali kwa klabu kufanya hivyo, na adhabu yake ni sawa na klabu hiyo kuvunja mkataba wa mchezaji huyo ndani ya klabu yake.
Tuachane na hayo, lakini usajili wa Tanzania tena kwa mchezaji mzuri kama Morrison, mambo huanza kama unavyoyasikia sasa, kama utani tu mwisho wa siku utasikia tayari ameshamwaga wino, ikitokea Ushishangae!
Lakini swali la msingi la kujiuliza, hivi ni kwanini Simba inaonekana kumtaka zaidi Morrison? Kwani Morrison ana vitu gani kiufundi ambavyo vitaisaidia Simba? Lakini pia lazima tujiulize, kwani Yanga hawamtaki Morrison? Acha tuanze na hili swali la mwisho.
Morrison ameongeza kitu gani ndani ya Yanga ya Luc Eymael?
Miongoni mwa dili linaloonekana la maana zaidi ni la kumnasa Mghana Bennard Morrison kutoka Orlando Pirates ya Afrika kusini,na kutua Jangwani Januari 15 mwaka huu kupitia dirisha dogo la usajili.
Kiufundi Morrison ni winga wa kulia na kushoto lakini pia anaweza kucheza kama mshambuliaji. Kiasili Morrison ni winga wa kulia lakini kasi yake inamfanya aweze kuonekana haraka akiwa katika eneo la ushambuliaji.
Kabla ya Ujio wake, Yanga iliingia na mfumo wa 4-4-2 ikianza na mawinga wawaili wa asili Patrick Sibomana na Deusi Kaseke au Ngasa, huku katikati akicheza Tshishimbi, Mapinduzi Balama na Niyonzima Haruna.
Chini ya Muangalizi Charles Boniface Mkwasa Master, yanga ilicheza kama ilivyo falsafa yake ya siku nyingi kushambulia kupitia pembeni.
Yanga ilishambuliaje? Ujio wa Morrison.
Yanga hutumia mabeki wake wa pembeni na mawinga kushambulia pembeni mwa uwanja, lakini hata hivyo Mkwasa aliingia na mpango kazi wa kushambulia kwa kutumia akili ya ziada kwa kuzingatia aina ya wachezaji waliopo na sifa zao.
Yanga ilianza na Juma Abdul upande wa kulia na jafary Mohamedi kushoto. Kisha upande huo huo wa kushoto ilianza na winga Patrick Sibomana. Kuanza kwa sibomana kulimaanisha Jafari asipande kushambulia kwa sababu sio mzuri wa kurudi haraka. Sibomana hakumuachia nafasi ya kushambua, badala yake alimlazisha asalie kama beki, na kumpa nafasi beki wa kulia (Juma Abdul) kushambulia.
Juma Abdul alishambulia vyema, kwa sababu Kaseke aliyecheza upande wake aliingia ndani na kuwa kiungo mshambuliaji, na kumpa nafasi Juma kushambulia kwa kupiga Krosi ‘mdondosho’. Muda huo wote, Washambuliaji wa kati, kazi yao ilikuwa ni kumalizia krosi za mawinga na mabeki wa pembeni pia kupokea pasi za mwisho kutoka kwa viungo.
Mbinu hii ilitumika katika michezo mingi aliyoisimamia Mkwasa kama kocha Muangalizi. Mfano katika mechi dhidi ya KMC msimu wa kwanza, Yanga ilipata sare ya 1-1 kupitia mbinu hii.
Yanga ndio iliyokuwa ya kwanza kupata goli dakika ya 73 kupitia kwa Mrisho Ngasa kabla ya Abdul Hillary kufunga kwa penati dakika za lala salama lakini kiujumla mechi nzima ilikuwa ni ya mbinu nyingi.
Baada ya kuachana na Juma Balinya na Sadney Urikhob, Yanga ikamsaka Morrison na kumpata, na kubadilisha kabisa mifumo ya kiuchezaji ndani ya Klabu na hata falsafa ya klabu inaanza kupotea, acha tuchimbe hapa kidogo…
Morrison aliingia moja kwa moja kwenye kikosi, na kucheza kama winga, wa kulia na kushoto. Morrison alitumia muda mwingi akitokea eneo la winga na kulisaka box la 18 la adui kwa kasi.
Tabia hii ilimfanya aizawadie Yanga faulo au penati na kushinda. Baada ya Emery kugundua kuwa anaweza kurahisisha kazi kwa kumuanzisha kama Mshambuliaji wa pili, Emery alifanya hivyo kwa baadhi ya mechi.
Vita kati ya Morrison na Sibomana.
Ujio wake, umeifanya Yanga kuua winga moja iliyotarajiwa kupiga Krosi. Patrick Sibomana alilazimika kuanzia nje, kumpisha Morrison. Sibomana na Morrison ni vitu viwili Tofauti kiufundi;
Sibomana anafunga lakini magoli yake mengi ni penati na faulo, Morrison anafunga magoli ya aina yote, Morrison anajua kuendesha mpira na kupiga vyenga kutoka eneo moja kwenda lingine, Morrison ana kasi ya kushambulia na kulitafuta Box la Mpinzani, anajua kupiga pasi na zikamfikia mlengwa, Muda wote anawaza jinsi gani anaweza kulifikia eneo la hatari la mpinzani.
Kiutamaduni Yanga sio timu ya kumiliki Mpira badala yake ni timu ya matokeo tu, lakini hivi karibuni Yanga inaonekana kuwekeza kwa wachezaji wenye uwezo wa kukaa na Mpira na kupiga pasi kama ilivyo kwa Haruna Niyonzima, Morrison, Mapinduzi Balama na Fei toto.
Ujio wa Morrison umeifanya Yanga ibadili mbinu ya kushambulia pembeni kwa kutumia mawinga wa asili na mabeki wa pembeni, badala yake Yanga hushambulia kutumia eneo moja la Uwanja kwa kutumia Krosi huku upande mwingine wa Morrison hushambulia kwa kasi kwa kutumia pasi fupi fupi na kupiga vyenga na kulifikia box la Adui.
Luc Emery humpanga Morrison upande Fulani kwa kuzingatia vitu vitatu:
Kwanza ni Kwa kuwaangalia mabeki wa pembeni anao anza nao upande wa kushoto na kulia. Endapo kama beki wake wa kulia hana uwezo mzuri wa kushambulia na kushuka haraka kulinda, Luc Humuweka Morrison upande huo lengo likiwa ni kumzuia Beki husika asishambulie wala kushambuliwa kwa sababu beki wa upinzani wakiungana na winga wake hawawezi kumuacha Morrison akiwa huru kutokana na uhatari wake.
Katika hili mara Nyingi, Morrison hujikuta akianza kwa upande wa kushoto kutokana na Udhaifu wa Jafary Mohammedi au Ally Mtoni Sonso kwa baadhi ya mechi kushindwa kutimiza majukumu yake kiusahihi ya kupanda na kushuka. Hii Humfanya Juma Abdul kubaki kama Mshambuliaji wa pembeni akisaidiana na winga wa upande wake.
Pili ni kutokana na mabeki wa pembeni wa timu Pinzani. Upande ambao ni hatari zaidi kwa Kushambulia kupitia pembeni ndio upande anaokaa Morrison.
Yaani kama beki wa kulia wa timu pinzani ni mzuri kwa ‘ku-overlap’, basi Morrison hucheza upande wa kushoto ili kumzuia beki huyo kupanda na kuishambulia timu kwa kutumia Krosi.
Na hiki ndicho kilichomfanya ang’ae dhidi Ya Simba, kwani mabeki wa Simba wote walikuwa wakipanda bila kuhofia uwepo wake, kiliwapata wote tunakijua.
Tatu ni aina ya Striker anayeanza. Hadi sasa yanga ina Mshambuliaji mmoja pekee mwenye uwezo kwa kubaki kati (standing striker) naye ni Yikpe. Wengine kama David Molinga na Ditraham Nchimbi ‘Duma’ wote hawakai eneo moja ni wazuri wa kucheza kama Mshambuliaji wa pili anayetokea kulia na kushoto akimuacha Mshambuliaji wa Mwisho kati kati ya mabeki wawili wa timu pinzani.
Luc akianza na Duma humuingiza pia Morrison kama Mshambuliaji wa pili anayetokea kulia na kushoto na kumlazimisha Duma kubaki kati kati kama Standing striker. Mfano katika mechi dhidi ya Simba, Morrison na Duma walicheza hivi na hata baada ya Morrison kutolewa hakukuwa na mwingine wa kumfanya abaki eneo la juu badala yake aliingia ndani kushoto na kulia ili kupokea mipira na kupanda nayo kushambulia kwa kasi.
Aina hii ya uchezaji ya Duma, bado anaitumia hadi leo pindi, Morrison anapokosekana na pindi, Yikpe anapoingia. Mfano katika mechi dhidi ya Mwadui na JKT Tanzania.
Huyo ndio Morrison! Lakini je akitua Simba kuna nini kitabadilika?
Acha tuitazame Simba inachezaje katika eneo la kiungo. Chini Sven Vandenbroeck Simba imekuwa ikitumia mifumo mingi ikiwemo 4-5-1, 3-5-2 na 4-4-2 iliyojibadili zaidi na kuwa 4-1-3-2.
4-1-3-2 ndio mfumo uliotawala katika kipindi cha Sven baada ya John Bocco kupona majeraha na kabla ya Jonas mkude kupata majeraha. Chini ya Mfumo huu Sven alianza na Mkude kama kiungo wa ulinzi, kicha Clatus Chama kama kiungo wa kati katika mstari sambamba na Luis Miquissone na Francis Kahata katika eneo la kati.
Chini ya Viungo hawa wanyumbulifu Simba ilimiki dimba, ilishambulia kwa kupiga pasi fupi fupi katika maeneo maalumu “positional play”. Katika aina hii ya uchezaji, Sven aliwategemea mabeki wa pembeni (Shomari Kapombe na Mohammedi Hussein kushambulia pembeni.
Mkude ndiye aliyekuwa Injinia wa mashambulizi kupitia pembeni kwani wakati Simba ikitumia eneo dogo kupiga pasi fupi fupi kulia au kushoto, Mkude alihamisha mpira kwa beki wa upande mwingine ambaye tayari huwa tayari amesha overlap pembeni na kushambulia kirahisi.
Mfano katika mechi ya ligi kuu dhidi ya Singida United, Mkude alifanya hivi zaidi ya mara moja kwa kuutumia upande wa Kapombe ambaye ni mzuri wa kuingia na mpira ndani ya boksi la Mpinzani na hata kupiga krosi, Simba ilishinda goli 8.
Simba ikianza na Miquissone na Kahata, ujue kabisa inaenda kumiliki dimba lakini ikianza na Hassan Dilunga na Deo Kanda ujue kabisa inaenda kushambulia pembeni.
Staili hii huwafanya Bocco na Kagere kubaki kati kati kwani Dilunga na Kanda huyatumia maeneo ya pembeni. Hii ni tofauti na wakianza Miquissone na Kahata kwani wote huingia katikati na kuwafanya Kagere na Bocco kuliacha eneo la kati na kuchezea maeneo ya wazi pembezoni mwa uwanja, hii huwakosesha Simba magoli mengi ukilinganisha na muunganiko wa Dilunga na Kanda kushambulia pembeni.
Mfano katika mechi dhidi ya Singida United Simba ilianza na Mkude kama kiungo wa ulinzi, kisha Miquissone kama kiungo wa kati huku Dilunga na Kanda wakicheza pembeni, Bocco na Kagere kama washambuliaji. Simba ilishinda 8, Kagere akifunga goli 4 peke yake.
Hivyo, kuna tofauti kubwa kwa Simba ikianza na Miquissone na Kahata (kama viungo wa pembeni wanaotokea kati) na Kanda na Dilunga (Kama mawinga) kwani katika mechi nyingi, Simba ikianza na mawinga hupata matokeo mazuri zaidi kuliko hata ikianza na viungo wa kati wanaotokea pembeni.
Ujio wa Morrison Simba.
Kama tulivyoona hapo awali kuwa Morrison ni winga mwenye kasi kubwa, hivyo kama atatua Simba maana yake anaenda kuongeza kitu kikubwa sana, kutokana na uwezo wake wa kupiga vyenga, kasi, kupiga pasi, kujiweka katika maeneo sahihi na kufunga magoli.
Ujio wake utaifanya Simba kushambulia maeneo yote ya uwanja, pembeni na hata katikati.
Vuta taswira hii…
Mkude kiungo wa ulinzi, Chama na Miquissone katikati, kanda na Morrison pembeni huku Kagere au bocco kama Mshambuliaji, Simba ikicheza 4-5-1, au Mkude na Chama katikati, Miraji Athumani na Morrison pembeni huku Kagere na Bocco kama Washambuliaji katika mfumo wa 4-4-2 lakini pia inaweza kucheza 4-3-3 kwa maana Miraji na Morrison wanaweza ungana na Mshambuliaji mmoja wa kati kuunda utatu wa maajabu. Unadhani ni nani atachomoka? Unadhani kuna mechi Simba itatoka sare ya kutofungana?
Asikudanganye mtu! Simba ina viungo wengi kuliko eneo lingine la kiuchezaji, ina viungo 14, tena wa kila aina lakini bado inamuhitaji Morrison kwa udi na Uvumba kutokana na upekee wake lakini pia kwa lengo la kupanua kikosi na kumpa kocha uwanja mpana wa kuchagua kikosi.