NIMEMFUATILIA kiungo mshambulizi wa Simba SC, Mzambia, Claytous Chama katika michezo kadhaa na kugundua mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Zambia ni muoga wa kupiga mashuti kutokana na kutokuwa fiti.
Chama alifunga goli lake la kwanza klabuni Simba siku ya jana Jumapili wakati Simba ilipoichapa Stand United 3-0 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Alifunga goli zuri kwa shuti la ufundi akiwa ndani ya eneo la hatari upande wa wing ya kushoto.
Kwa nafasi yake- kiungo mchezesha timu, Chama anatakiwa kufunga walau kuanzia magoli matano ili Simba iweze kutetea ubingwa wao msimu huu.
ANAOGOPA!
Mara kadhaa kiungo huyo amekuwa akipata nafasi za kushuti lakini hafanyi hivyo. Nadhani atakuwa anahofia kutonesha maumivu ya enka ama goti ndiyo maana hata pale anapopata nafasi Nzuri ya kupiga shuti hafanyi hivyo zaidi ya kulazimisha kutoa pasi kwa mchezaji mwenzake.
Kikawaida mchezaji aliyeumia mara mbili ama zaidi eneo lake la enka ama goti anapopona hata kama alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti ya mbali, taratibu huanza kupoteza ujasiri huo kutokana na hofu ya kujitonesha.
Kiuchezaji- Chama hatofautiani sana na nahodha wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto. Kwa anayemfahamu Kazimoto tangu wakati yupo Ruvu Shooting mwaka 2008 atakuwa ni shahidi wa hili nisemalo.
Kazimoto licha ya kwamba ni mahiri katika kutawanya pasi, kumiliki mpira na uwezo wa kupiga pasi za mwisho, sifa yake nyingine ilikuwa ni uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali yenye mwelekeo golini mwa wapinzani wake.
Lakini mara baada ya kiungo huyo wa zamani wa Taifa Stars kupata maumivu makubwa ya enka Julai, 2011 amekuwa muoga wa kupiga mashuti na hata anapofanya hivyo kwa sasa huwa hatumii nguvu nyingi kama wakati ule hajaumia.
Kwa kumtazama Chama anavyocheza hapana shaka ni mchezaji mzuri. Anachezesha vizuri timu yake, ana jicho la kupiga pasi Safi za mwisho lakini anaonekana kuwa na hofu fulani wakati wa kupiga shuti na hii inaweza kuchangiwa na majeraha ambayo amewahi kuyapa huko nyuma.
Katika ligi, ili mfanikiwe kushinda ubingwa wakati mwingine timu inatakiwa kufunga walau goli moja tu. Na kuna wakati mchezoni unajikuta huwezi kupata goli hilo litakalowapa alama tatu kutoka kwa washambuliaji. Ni hapo ndipo unahitaji kiungo/beki kukufungia goli hilo muhimu.
Kama Chama yupo fiti basi kocha wake Patrick Aussems anapaswa kumwambia ajitahidi kadri ya anavyoweza kupiga mashuti yenye mwelekeo golini mwa wapinzani wao vinginevyo wataangusha sana pointi mbele ya timu zinazojilinda vizuri katika eneo lao la hatari.
Kutegemea magoli kutoka kwa washambuliaji pekee kutawaangusha na ili wasianguke ni lazima mchezesha timu kama Chama afunge walau magoli matano ambayo yanaweza kuwapa alama 15.