Unafuatilia soko la wachezaji muda huu?, soko limechafuka pesa sana. Pesa zinasafiri kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.
Na kuna wakati pesa hizi zinasafiri kutoka bara moja kwenda bara jingine. Hii yote ni kuonesha namna ambavyo bidhaa mchezaji ilivyo na umuhimu sana.
Kipindi hiki watu hawapati usingizi ulio bora wakiwaza namna ya kupata wachezaji bora, mawakala nao wanawaza kutengeneza pesa kupitia wachezaji.
Na kuna wakati pia vilabu navyo vinawaza jinsi ya kutengeneza pesa kupitia hawa wachezaji wanaowamiliki.
Hiki siyo kitu cha kushangaza sana kwa sababu tu kuuza wachezaji ni njia nyingine kubwa ya klabu kuwa kama chanzo cha kipato.
Unaweza ukawa na wadhamini kwenye klabu yako, ukawa unauza bidhaa zenye nembo ya klabu yako. Ukawa unawachama wanaolipia kadi zao na ukawa unajaza viwanja lakini kuuza wachezaji ni chanzo kingine kikubwa cha kipato.
Kwa bahati mbaya sana hapa kwetu hii biashara haijaangaliwa sana kwa kiasi kikubwa. Vilabu vyetu vinawaza kutumia pesa kwa ajili ya kusajili.
Hakuna klabu ambayo imeshawahi kuwaza kuzalisha wachezaji bora ambao wataipa timu mafanikio ndani ya muda fulani na baadaye kuwauza kipindi ambacho timu imenufaika na mchezaji.
Na wakati mchezaji anauzwa kunakuwa na mchezaji ambaye anakuwa tayari ameshatengenezwa kwa ajili ya kuziba pengo la huyo mchezaji.
Aliwahi kuondoka Fernando Torres, Diego Forlan alifuata, akaja Sergio Aguero, akaja Diego Costa na leo hii tunaona Atletico Madrid wanatengeneza pesa nyingi kwa kumuuza Antoinne Griezmann.
Wote hao waliondoka waliipa mafanikio Atletico Madrida na Atletico Madrid waliwauza kwa bei kubwa, bei ambayo wao waliingiza faida kubwa.
Na kila aliyekuwa anauzwa walihakikisha wanamtafuta mchezaji ambayo ni bora katika eneo hilo la ushambuliaji.
Walifanya biashara huku wakinufaika na matokeo ndani ya uwanja. Yani kwa kifupi walikuwa wanapata faida ndani ya uwanja kwa hao wachezaji kuisaidia timu na mwisho wa siku wakapata faida ya fedha.
Hii ndiyo biashara halisi ya mpira, biashara ambayo kwetu haitaki kuangaliwa kwa kiasi kikubwa. Bajeti ya vilabu vyetu kwa mwaka ni wastani wa bilioni moja.
Bajeti ambayo ni kubwa kwa kuangalia ila ni ndogo kwa uhalisia kwa sababu ukiamua kufanya uwekezaji eneo hili la biashara ni wachezaji wawili au watatu wanaweza kukupa hiyo pesa.
Kuliibuka habari za chini chini za Makambo kuuza Horoya FC ya Guinea kwa dau ya milioni 300, dau ambalo mpaka sasa hivi hatujui kama limeenda kwa Yanga.
Kwa dau hili ukiamua kuwekeza kwa wachezaji watatu wanaweza kukusaidia na kuachana na habari za kuchangiwa na wanachama.
Hii ni biashara kubwa sana, biashara ambayo imenifanya nijifikirishe leo asubuhi kama pesa za Makambo , Yanga wamezipata au la!.