Tarehe 21, Machi 1980 kunako mji wa Port Alegre nchini Brazil mtoto Ronaldo de Assis Moreirra alizaliwa, mzee Joao Moreirra na mkewe Bi Miguerina De Assis walifanikiwa kumzaa mtoto ambaye baada ya miaka kadhaa kupita alifanikiwa kuwa mwandinga maarufu
Jina lake halisi anaitwa Ronaldo lakini wabrazil ili kumtofautisha na Ronaldo de Lima waliamua kumwita Ronaldinho wakiwa na maana Ronaldo mdogo, Ronaldinho tangu akiwa na umri wa miaka saba tayari alianza kuwa gumzo katika mtaa wao kutokana na uwezo mkubwa kabisa wa kusakata kabumbu, hii ilitokana na yeye kuzaliwa kwenye familia ya wanandinga na hapa ndipo ninapokumbuka usemi wa waswahili kuwa cha kurithi uzidi
Mzee Joao Moreirra ambaye ni baba mzazi wa Ronaldinho Gaucho na kaka yake wote walikuwa wacheza soka, japokuwa hawakuweza kutamba kama mtoto wao lakini hii inadhihirisha kwamba haikuwa ajabu kwa Gaucho kuwa mcheza kabumbu mashuhuri ulimwenguni
Alianza kucheza soka akiwa bado mdogo sana na mara nyingi alipenda kucheza na watu wenye umri mkubwa zaidi yake na wengi waliomuana walishangaaza na uwezo wake, na kama ilivyo kawaida kwa wanasoka wengine wa Kibrazil Ronaldinho Gaucho naye alianza kwa kucheza samba mtaani kwako kisha baadae akaonekana na kupelekwa kunako klabu ya Gremio hapa ndipo alipoanza kuvaa viatu vya Nike ilikuwa mnamo mwaka 1998
Katika mwaka uliofuta Gaucho aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil, iliyokuwa ikienda katika michuano ya kombe la mabara ambapo katika hiyo Brazil ilimaliza kwenye nafasi ya pili huku Gaucho akiibuka mchezaji bora wa michuano hiyo
Baada ya kutamba sana kunako klabu ya Gremio, hatimae Gaucho alijiunga na klabi PSG ya Ufaransa hapa ndipo mahala ambapo unaweza sema uimwengu wa soka ulikuwa umesogezewa kiumbe mwenye uwezo wa kuiita mpira na kufanya anavyotaka, hakika mpira ulimtii kwenye miguu yake.
Gaucho alifanya mambo makubwa sana kwenye klabu ya PSG kiasi cha kuvifanya vilabu vingine kuanza kumtolea macho, akiwa anatamba sana ya Ufaransa ndipo mwaka 2002 ndipo Gaucho alikwenda kwenye michuano ya kombe la Dunia iliyofanyika Korea kusini na Japan hapa alifanikiwa kubeba kombe la Dunia akiwa ni timu yake ya taifa ya Brazil, ambapo alifanikiwa kufanga mabao 2 katika mechi 5 alizocheza
Gaucho alimfunga goli la aina yake kipa mkongwe wa Uingereza David Seaman, kwenye michuano ya kombe la Dunia huko Korea kusini wakati Brazil ikicheza na Uingereza ikiwa ni kwenye mchezo wa robo fainali, Gaucho akiwa na Livaldo, Ronaldo de Lima kwenye eneo la ushambuliaji waliifunga Ujermani kwenye mchezo wa fainali na kubeba kombe hilo
Mwaka 2003 alihamia kuna klabu ya Barcelona, hapa ndipo mahala ambapo aliweza kujitambulisha sana kwenye ulimwengu wa wapenda soka anakutana na Samuel Et’o, Deco de souza kwa pamoja wanaanzisha kile walichokishindwa kina Luis Enrique, Luis Figo na Patrick Kluivert hatimae Camp nou inakuwa nyumba ya mataji
Akiwa Barcelona anafanikiwa kubeba makombe kibao pia kuufanya mchezo wa soka kupendwa zaidi, itakumbukwa mwaka 2005 katika mchezo wa ligi ya mabingwa ulaya uliofanyika kunako dimba la Stamford bridge Chelsea wakipata ushindi wa mabao 4-2 dhidi Barcelona, Gaucho alifunga bao huku akicheza samba kwa mtindo wa kukata kiuno nje kidogo ya eneo la 18 kisha akautupia mpira wavuni na kuwaacha nahodha wa Chelsea wakati huo John Terry na kipa Petr Cech wakiwa hawajui cha kufanya
Barcelona ndipo mahala ambapo Ronaldinho alishinda karibia kila kitu, alibeba mataji mawili ya ligi, akabeba Balon d’or mwaka 2006 pia akabeba taji la ligi ya mabingwa ulaya
Baada ya Frank Rijikaard kuondoka Barcelona na kuja kwa Pep Guardiola ndiye alikuja kumuuza Gaucho kwenda Ac Milan ya Italia, ambako ilishuhudiwa wakibeba ubingwa wa serie A msimu wa 2010/11 na msimu huo huo Ronaldinho akatemwa timu ya taifa ya Brazil
Maisha ya soka ya Ronaldinho yalianza kuyumba alikwenda Atretico Mineiro ambapo katika michezo 85 alifunga mabao 27, Quretatro ya Mexico alifanikiwa kufunga mabao 8 na kunako klabu ya Fluminense hakufunga bao hata moja
Ronaldinho licha ya kuwa mshindi wa tuzo ya Balon d’or mwaka 2005, pia ameshinda tuzo ya Fifa World player of the year mara mbili mfululizo 2004 na 2005 na akajuimshwa kwenye kikosi bora Uefa cha mwaka kwa mara tatu mfululizo 2004, 2005 na 2006
Mara ya mwisho kwa Ronaldinho kucheza soka la ushindani ilikuwa mwaka 2015 akiitumikia klabu ya Fluminense, pia Gaucho ameichezea timu ya taifa ya Brazil michezo 97 na kufanikiwa kufunga mabao 33
Hii leo kaka wa Gaucho aitwaye Roberto Assis, amethibitisha kuwa mwisho wa ndugu yake kutumikia mchezo wa soka umefika na wao kama familia wanajipanga kufanya tukio la kumuaga
Na mimi nasema kwa heri fundi wa mpira, waswahili husema wakati ni ukuta