Simba walipita kina Victor Costa, Juuko Mursheed, Pascal Wawa, Joash Onyango na sasa wamempata Che Fonde Malone kutoka Cameroon.
Malone ametoka Cotton Sports huku akitoka kuwa MVP yaani mchezaji bora wa msimu uliopita. Si hilo tu lakini rekodi zinaonyesha tayari ameshaanza kuitwa timu ya Taifa ya Cameroon na kucheza baadhi ya mechi.
Yote hayo yanakuonyesha Simba hawakutoa zaidi ya dola laki moja kwa bahati mbaya ili kumnunua kutoka kwa wababe hao wa Cameroon, pia tunaambiwa alikuwa na ofa za kutoka Ulaya pia.
Tayari amecheza na nimemuona katika michezo miwili, ule wa kirafiki dhidi ya Power Dynamos na ule wa Ngao ya hisani dhidi ya Singida Fountaine Gate Fc na itoshe kusema huyu ni beki haswa tena mlinzi wa kati wakisasa.
Che Malone tayari ameonyesha ana uwezo mkubwa katika eneo lake kama mlinzi wa kati akionyesha uwezo mkubwa katika kucheza kuanzia nyuma, kucheza mipira ya juu na hesabu nzuri katika kuwadhibiti washambuliaji. Japo bado sina hakika kama anauwezo mkubwa katika kuwakabili washambuliaji wenye kasi.
Kwa modern football inayohitaji kuanza kucheza kuanzia nyuma basi kwa Malone ndio penyewe kwani ana utulivu mkubwa na uwezo mkubwa wakupiga pasi hata kama akiwa katika presha ya mpinzani.
Che pia si tu katika kucheza lakini katika kutimiza jukumu lake lakwanza la ulinzi yupo vyema, ana “timing” nzuri katika mipira yakugombea, ana mahesahu mazuri katika mipira ya hewani lakini pia yupo “aggresive” katika kupambana na mshambuliaji wa timu pinzani.
Tayari muunganiko wake na Inonga Bacca ni kama umeanza kulipa hivi kwa Simba, lakini kupatia kwao ni muendelezo mwingine wa mauvu kwa Kenedy Juma na Hussein Kazi mabeki wetu wakati wazawa hawa.