Huku ligi kuu bara ikipamba moto timu bado zinapambana haswaa na kufanya kuzidi kunogesha na kuonyesha utamu wa ligi yenyewe.
Timu za Simba, Yanga, Azam na Singida utd zikipambana nafasi za juu kuwania ubingwa, upande wa pili huku kuna Majimaji, Njombe Mji, Kagera Sugar, Ndanda, Mbao na Mwadui zikipambana na hali yao kuepuka kushuka daraja.
Utamu wote huu na ushindani wa VPL kwa kiasi kikubwa unatokana na wadhamini wakuu Vodacom na AzamTV, ambao haswa wamesaidia mwendelezo mzuri wa ligi yetu.
Ligi ili iwe na ushindani kwa timu zote inahitaji maandalizi mazuri kuanzia kwenye usajili, pre-season na kambi nzuri ya timu. Vitu vyote hivyo vinahitaji matumizi makubwa ya fedha.
Kwa kiasi kikubwa timu zote 16 zinazoshiriki VPL zimekua zikitegemea mapato ya mlangoni na fedha kutoka kwa wadhamini wakuu ambao ni Vodacom na AzamTV.
Hivyo kupelea kwa kiasi kikubwa kushindwa kuendana na maana halisi ya soka la ushindani na kufanya kushindwa kulipa mishahara na posho, kushindwa kuweka kambi na maandalizi mazuri ya timu, kulipa pesa za usajili na kupelekea mara kwa mara wachezaji kugoma.
Mara kwa mara timu zimekua zikilia kukosa pesa hivyo kujitahidi kutafuta wadhamini huku na kule ili kujitahidi kuendana na matumizi ya timu. Pesa za wadhamini wakuu ambazo zimekua zikitolewa zimekua hazitoshi.
Kutafuta na kupata wadhamini imekua changamoto kwa timu zetu haswa timu ndogo ukiondoa timu za Simba, Yanga na Azam.
Nini kinaweza kumvutia mdhamini katika klabu yoyote ile? Hili ni swali ambalo meneja masoko yeyote wa timu anaweza jiuliza.
“Utulivu wa klabu na uongozi imara wenye mipango ambayo inaashiria kukuza soka na wapo kibiashara pia, kwangu mimi naona ndio mazingira tosha kupeleka udhamini wangu“
-Nassor Binslum,Mkurugenzi wa kampuni ya Binslum.
Viongozi wa vilabu hivi ni wajibu wao kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji, kwa kuwa na mipango madhubutu yenye manufaa kwa pande zote mbili (Mdhamini na Klabu) kwa manufaa ya klabu na mashabiki wake.
Kwa sasa kwa kiasi kikubwa mambo yamebadilika angalau neema imeongezeka na vilabu vidogo kupata wadhamini na kusaidia katika upatikanaji wa fedha na kuendesha timu. Moja ya faida ya udhamini huu, matangazo yao sasa yanaonekana mubashara katika luninga, pongezi kwa ujio wa Azam TV katika soka la Tanzania.
Kinachohitajika pia kwa vilabu vyenye udhamini au vinavyotafuta, ni kuheshimu maana ya udhamini na ‘branding’. Mfano wahusika wanaodhaminiwa na Biko Sports hawatakiwi kuonekana wamevaa Sokabet, hii inamlinda mdhamini.
Angalau sasa kwenye ligi timu nyingi zimepata udhamini na kupendezesha jezi zao kifuani huku mifukoni kukiwa na ahueni. Hata zile timu zinazoonekana ndogo pia zimefanikiwa kupata udhamini.
Timu kubwa kama Yanga na Simba zina mdhamini wao Sportpesa, Azam wapo na NMB na Singida utd wakiwa na YARA, Azania Bank na Sportpesa.
Stand utd wapo na udhamini wa BIKO Sports na Jambo, Majimaji FC wanadhaminiwa na Sokabet, Mbeya City wana udhamini wa Binslum (RB Batery) na Cocacola,.
Ruvu Shooting wanadhaminiwa na Cowbell milk, Mbao FC Wakiwa na wadhamini wawili Cowbell na GF Trucks and Equipment LTD.
Timu za Mwadui fc, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Njombe Mji, Lipuli, Ndandafc na Tanzania Prisons ndio timu pekee zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zikiwa hazina mdhamini.
Kwa idadi ya timu zinazoshirki VPL na idadi ya timu zenye wadhamini angalau tunasogea kule tunapopaota kila siku, kwenye kujenga ligi bora na yenye ushindani, mana siku hizi wanasema “Mpira Pesa”.
Hivyo bodi ya ligi kwa kushirikiana na TFF kupitia kitengo cha masoko wajitahidi kuzidi kuipa thamani na ”Kui-Market” ligi yetu ili izidi kuvutia wadhamini kwenye vilabu vyetu, ikiwa ni pamoja kulegeza au kuboresha vigezo ili kuruhusu makampuni yanayotoa huduma sawa na mdhamini mkuu kudhamini vilabu.
Pia kwa Maafisa masoko wa vilabu vyote ni vema basi tukajitahidi ”Kubrand” timu zetu ili kuweza kuvutia wadhamini wa ndani na nje ya nchi kuja na kudhamini timu zetu na kusaidia kuongeza fedha kwa timu. Hili litapelekea vilabu kutokutegemea makusanyo ya milangoni au kutembeza mabakuli kwa wapenzi na wanachama wao.