EMMANUEL Amunike alifanya mabadiliko matatu katika kichapo cha 1-0 ambacho timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) ilikipata katika mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Misri usiku wa jana, lakini nyuma ya kipigo hicho kuna matatizo kadhaa yameonekana katika kikosi chake ambacho kinajiandaa na fainali za kombe la Mataifa ya Afrika zinazotaraji kuanza kutimua vumbi lake Juni 21 nchini Misri.
BEKI ZA PEMBENI….
Hassan Kessy Ramadhani alianza na kumaliza mchezo kama beki wa kulia, Gadiel Michael akianza katika beki tatu. Hawa ndiyo walinzi chaguo la kwanza katika timu tangu ilipokuwa chini ya Amunike miezi sita iliyopita.
Walinzi hao licha ya kwanza wana pumzi na uwezo wa kupandisha mashambulizi, kukosa kwao utulivu hasa wakati wakipiga pasi ya mwisho ni tatizo ambalo Amunike anapaswa kulifanyia kazi kabla ya kuwavaa Senegal katika mchezo wa kwanza.
Walizuia vizuri, na kuna wakati walikuwa wakipandisha timu kwa nguvu katika sehemu za pembeni na kurudi haraka kuzuia lakini kama wanapanda na kuishia kupiga pasi-krosi zisizo na macho inaweza kuwaletea matatizo kila wakati katika nafasi zao. Walinzi hao kwa sasa tayari wanao uzoefu wa kutosha hivyo wanapaswa wao wenyewe kabla ya mwalimu kujisahihisha haraka.
BOCCO SI MSHAMBULIZI WA PEMBENI
Amunike alianza mchezo wa jana kwa kuwapanga nahodha Mbwana Samatta na John Bocco katika eneo la mashambulizi. Katika mfumo wa 4-4-2, Himid Mao na Feisal Salum walicheza kama viungo wa kati, Saimon Msuva katika wing ya kulia na Farid Mussa katika wing ya kushoto. Wachezaji hawa watano ( ukiachana na Feisal) wamecheza pamoja kwa muda usiopungua miaka mine sasa hivyo Amunike anaweza kutumia maelewano yao kuifanya Stars ipate magoli.
Licha ya kuonekana katika mfumo Bocco akicheza nafasi ya kati, lakini kiuchezaji Amunike inaonekana alimwambia atokee pembeni Zaidi na eneo la kati alionekana Zaidi Samatta. Kwa aina ya kiwango chake kwa dakika 62’ alizokuwa uwanjani Bocco hakuonekana kuwa na msaada mkubwa katika ufungaji kwa sababu, Bocco si mzuri kutokea pembeni na kukimbilia kati.
Kama, Amunike anaona upo msaada Bocco anaweza kuutoa kwa timu yake basi ampe uhuru straika huyo na Bocco huwa mkali Zaidi anapotokea kati na kukimbia pembeni.
SAMATTA NI NAMBA 10
Ni, Jan Poulsen pekee ambaye aliweza kumtumia vizuri Samatta lakini kuanzia kwa Kim Poulsen, Martin Noorj, Charles Mkwassa, Salum Mayanga na sasa Amunike wote hawa wamekuwa wakishindwa kumsaidia Samatta kufikia kiwango cha juu akiichezea Stars kwa sababu wamekuwa waking’ang’ania kumchezesha mshambulizi huyo wa KRC Genk kama mshambulizi wa kwanza.
Samatta hupendelea kucheza namba kumi kwa sababu hupata eneo kubwa la kukokota mpira na kujitengenezea nafasi za kufunga. Kwa timu ambayo haina kiungo bora mchezesha timu na mwenye jicho kali la upigaji wa pasi za magoli Stars inamuhitaji Samatta huyu aliye katika ubora wa juu sasa kufunga walau magoli mawili katika michezo mitatu ijayo ya makundi.
Thomas Ulimwengu ambaye alichukua nafasi ya Bocco alionyesha jinsi gani Stars ‘itasafa’ katika ufungaji na umefika wakati sasa wa Amunike kumpa nafasi Rashid Mandawa kwa mara ya kwanza katika mchezo ujao wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe.
Mandawa naamini ana uwezo mkubwa wa kusimama kama mshambulizi pekee na kudhibiti mipira ya chini ya ile ya juu, uwezo wake unaweza kumfanya Samatta awe huru Zaidi kuhaha kusaka mabao na kutengeneza nafasi za kufunga. Mandawa hajawahi kucheza mchezo wowote Stars chini ya Amunike licha ya kwamba amekuwa akiitwa na kocha huyo Mnigeria kila anapotangaza kikosi chake.