Mchezo wa kwanza tu kuzalisha magoli mengi ndani ya dakika 90, Shirikisho la Soka nchini-TFF limeonyesha udhaifu mkubwa. Mshambulizi wa Stand United, Alex Kitenge ambaye alifunga magoli matatu kwa mpigo ‘Hat Trick’ wakati timu yake ilipochapwa 4-3 na Yanga SC siku ya Jumapili iliyopita ‘alinyimwa’ mpira aliopaswa kupewa na mwamuzi mara baada ya kumalizika kwa mchezo.
Kawaida, mchezaji anapofunga magoli matatu au zaidi katika mchezo mmoja huzawadiwa mpira uliotumika katika mchezo husika mara baada ya kumalizika, lakini kwa mara ya kwanza katika karne mpya, mfungaji wa Hat Trick ananyimwa mpira huku TFF ikisema haiwezi kumpatia kwa sasa kwa sababu wana idadi ndogo ya mipira.
Wiki mbili zilizopita niliandika makala na kuzitaka klabu zinazoshiriki ligi kuu msimu huu kugoma kuendelea kucheza ligi hiyo hadi pale Shirikisho litakapowaambia nini hasa washindi wa ligi hiyo watapewa mwishoni mwa msimu. Hii itaepusha ulalamishi wa zawadi zisizostahili mwishoni mwa msimu.
Inafahamika ligi hii ya sasa haina mdhamini hivyo Shirikisho na klabu zote 20 kila moja kwa nafasi yake anapaswa kuwajibika katika nafasi zao. Klabu kujigharamia usafiri, malazi na vifaa vya kutumia. TFF nao wanapaswa kuiendesha ligi na kuifanya yenye hadhi ya ligi kuu. Wanapaswa kugharamikia zawadi za washindi, waamuzi na wasimamizi.
Najiuliza kama mfungaji wa magoli matatu katika mchezo mmoja ananyimwa mpira kwasababu TFF haina ya kutosha, itakuwaje siku watakapotakiwa kutoa zawadi za bingwa na washindi wengine wanne wa juu katika ligi, mfungaji bora, kipa bora, mwamuzi bora, kocha bora, timu yenye nidhamu na nyingine kama zile za mchezaji bora wa mwezi?
Tunapaswa kutazama matukio kama haya yanayoonekana madogo madogo lakini tukumbuke kuwa huu ndiyo uhalisia wenyewe na sasa tupo katika ligi ambayo hata mfungaji wa Hat Trick hawezi kuzawadiwa mpira, bingwa na washindi wengine hawajui watapata zawadi gani! Kunyimwa mpira kwa Katenge ni kichekesho lakini kinapaswa kuziamsha klabu na kuungana kuuliza nini hatma ya washindi.
Ningekuwa katika nafasi ya Wallace Karia ningejiuliza kwanza, ‘mwaka mmoja tangu niingie madarakani, nimefanikiwa au nimeurudisha nyuma zaidi mpira wa Tanzania na kufikia maamuzi, si mengine ni kujiuzulu tu.’