Sambaza....

Sikubahatika kwenda uwanjani kwenye mechi ya ngao ya jamii kati ya Simba na Azam FC, lakini nilitumia muda mwingi sana kuitazama mechi hii.

Mechi ambayo ilikuwa na burudani sana ndani ya uwanja. Burudani ambayo ilitokana na timu zote kutaka kuuchezea mpira.

Hawakuwa na muda wa kufikiria kukaa nyuma ya mpira muda wote, wachezaji wa timu zote muda mwingi miguu yao ilikuwa inatamani kuwa na mpira.

Hapa ndipo utamu wa mpira ulipoanzia. Kila mtu anautaka mpira, mchezo ukawa wa wazi sana. Kila mtu akapata nafasi ya kucheza atakavyo.

Mpira ulinyanyaswa sana. Na haikushangaza Azam FC kuwa watu wa kwanza kufunga goli. Goli ambalo lilinifanya nione Simba Sc kwa sasa inaendeshwa kitaalamu.

Simu yangu haikuwa mbali sana na mikono yangu wakati natazama ile mechi, na sikusita kuingia kwenye ukurasa wa Twitter wa Simba.

Unajua nilikutana na nini ?, nilikutana na kitu cha ajabu ambacho sikuwahi kukiona kabla kwenye vilabu vyetu hapa nchini, labda vilabu vya ulaya!.

Ukurasa wa Simba wa Twitter ulikuwa umetoa matokeo ya mechi iliyokuwa inaendelea ambapo Azam Fc ndiyo walikuwa wanaongoza!

Maajabu !, kurasa nyingi za mitandao ya kijamii za timu zimegeuka mitandao ya kutoa matokeo, na siyo kinachoendelea uwanjani, labda tu wafunge wao.

Ni ngumu kwa timu kutoa matokeo kwenye mitandao yao wanapofungwa. Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza naona kwa Simba.

Simba ambayo amefanya mabadiliko makubwa kwenye idara yake ya habari. Imeajiri mpaka mtu wa kushughulikia mitandao pekee.

Mitandao ambayo kwa sasa inaendeshwa kwa weledi mkubwa. Hutopata dhambi yoyote kama ukisema Simba kwa sasa inajiendesha kwa weledi kwenye mitandao ya kijamii kuzidi timu zote hapa nchini.

Simba inajiimarisha ndani na nje ya uwanja. Wanamaanisha wanachokidai. Wanadai mafanikio kweli kweli.

Hatua zao za kupigania mafanikio zinaonekana ni za uhakika sana. Hawabahatishi ndiyo maana hata timu yao ni bora sana.

Inacheza vizuri, ina wachezaji bora kwenye kila idara. Kwa kifupi Simba inafanya vizuri ndani na nje ya uwanja. Na bila shaka timu nyingi zinatamani sana kuwa kama Simba.

Sambaza....