Nadhani ni wakati wa TFF na Bodi ya Ligi (TPLB) kuwa na tuzo maalum kwa wachezaji wetu wanaocheza nje katika usiku wa tuzo za ligi msimu huu. Ina maana kubwa.
Mataifa mengi yana utaratibu huu. Kunakuwa na tuzo za msimu kiujumla, kisha kunakuwa na tuzo za wachezaji wa nchi husika wanaocheza nje ya nchi yao. Hii itawahamasisha katika kazi zao na kuwajengea heshima huko wanakocheza.
Vipi leo Kelvin John “Mbappe” akipewa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Tanzania kwa wanaocheza nje? Ni kitu kikubwa kwake. Poa ni kitu kikubwa kwetu kama Taifa. Nashauri tuwe na tuzo za namna hii. Iwe msimu huu, iwe msimu ujao. Hizi tuzo zina maana kubwa.
Zamani tulikuwa na kundi dogo la wachezaji wanaocheza nje. Hawakuwa wanafika hata watano, lakini hivi sasa tunaweza kuita wachezaji 17 wanaocheza nje bila kujumuisha wachezaji wa ndani. Hii peke yake inamaanisha tayari tuna wachezaji wengi nje.
Himid Mao Mkami ana zaidi ya miaka mitano sasa pale Uarabuni. Huyu alipaswa kuwa na tuzo. Captain Diego Mbwana Samatta ndiye Mussa wa mpira wetu aliyechapa maji na watu wengine kuvuka, huyu alipaswa kuwa na tuzo maalum.
Vipi kwa Novatus Dismas, Simon Msuva, Emilian Mgeta, Mourice Abraham? Wako vijana wetu wengi. Hawa tunapaswa kuwatia moyo kwa kuwapa tuzo. Tukiwa na utaratibu huu, tutawahamasisha vijana wengine nao kwenda nje.