Ni kama homa ya Kombe la dunia inazidi kupanda huku makocha wa timu za Taifa wakitangaza vikosi vyao vya wachezaji 23 watakaounda timu zao.
Baadhi ya timu zimeshatoa majina ya wachezaji wake 23 watakaoziwakilisha nchi zao, huku baadhi ya majina makubwa yakikosekana kwenye vikosi hivyo.
Kuna nyota mbalimbali wanaokosa michuano hiyo mikubwa kwa sababu mbalimbali. Baadhi yao wanakosa kwa sababu ya majeruhi lakini wengine kwa sababu ya kuzidiana uwezo na wachezaji wengine wanaoitwa kwenye vikosi vyao.
Tovuti yako ya kandanda inakuletea kikosi cha wachezaji 11 wanaokosa kombe la dunia:
1. Joe Hart – England (West Ham)
Ujio wa David Moyes ni kama ulisababisha akose kombe la dunia baada ya kuamua kumtumia kipa namba mbili na yeye kukaa bechi.
Nafasi yake imechukuliwa na chipukizi Pickford wa Everton.
2. Dani Alves – Brazil ( PSG)
Alipata majeraha akiwa na klabu yake ya PSG hivyo kushindwa kujumuishwa katika kikosi cha Seleção. Nafasi yake imechukuliwa na Danilo wa Manchester City.
3. Alex Sandro – Brazil ( Juventus)
Amekua na msimu mzuri na Juventus kama beki wa kushoto, lakini ni ngumu kwake kupenya katika kikosi mbele ya Marcello na Philipe Luis.
4. Laurent Konsielny – France (Arsenal)
Alipata majeraha akiwa kwenye mchezo wa Europa League dhidi ya Athletico Madrid na hivyo kuzima ndoto zake za kujumuishwa katika kikosi cha Ufaransa. Nafasi yake imezibwa na Kimpembe wa PSG.
5. Cris Smalling – England (Man Utd)
Amepata nafasi kubwa ya kucheza mbele ya Phil Jones wakiwa Manchester lakini ni kama hakua na bahati baada ya nafasi yake kupewa Gary Cahill wa Chelsea.
6. Adel Rabiot – France ( PSG)
Sio uwezo bali tuu ni jinsi timu ya Ufaransa ilivyobarikiwa vipaji na haswa eneo la kiungo. Nafasi yake imezibwa na Tolliso wa Bayern Munich.
7. Mario Gotze – Germany (B. Dortmund)
Mfungaji wa goli lililoipa Ujerumani ubingwa mbele ya Argentina mwaka 2014 huko Brazil. Nafasi yake imechukuliwa na rafiki yake Marco Reus walio timu moja Dortmund.
8. Fabinho – Brazil ( Monaco)
Kiraka wa Monaco amekosa nafasi mbele ya wachezaji kama Fernandinho, Paulinho na Casemiro wanaocheza nafasi ya kiungo wa ulinzi Kama yeye.
9. Karim Benzema – France ( Real Madrid)
Ni skendo za nje ya uwanja ndizo zilizomfanya asiitwe timu ya Taifa na sio uwezo wake wa uwanjani. Nafasi yake imezibwa na Thuavin wa Olimpique Marseille.
10. Jack Wilshere – England (Arsenal)
Ni kama hana bahati hivi katika maisha yake ya mpira baada ya kuwa fiti msimu mzima lakini kocha wa Uingereza alichagua kumuita chipukizi Loftus Chick na kumuacha yeye.
11. Anthony Martial – France ( Man Utd)
Nafasi yake imechukuliwa na Thomas Lemar wa Monaco huku akiwaachia gumzo wapenzi wa soka ni kwanini hajajumuishwa katika kikosi cha Ufaransa. Huku wachambuzi wengi wakihoji uwezo wa uchaguzi wa mwalimu wa Ufaransa.