Wananchi Yanga kesho jioni wanashuka uwanjani katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants na kuelekea mchezo huo kocha wa Yanga amesema watatumia akili zaidi.
Kocha mkuu wa Yanga Nasradinne Nabi kuelekea mchezo huo amesema “Ni mechi inayohitaji akili na tahadhari kubwa sana, tunacheza mechi ya nyumbani lakini haiwezi kufuzu kwa mchezo mmoja, ni lazima tucheze tukiwa tunawaza dakika 180 za nusu fainali yote.”
Yanga ambao ndio vinara wa Ligi Kuu ya NBC wanakwenda kukutana na Marumo ambayo haifanyi vyema Ligi ya kwao Afrika Kusini, PSL wakiwa katika eneo la timu zinazoshuka daraja lakini kocha wa Yanga amesema hilo wala halipo kwenye hesabu zake.
Nabi amesema yeye ameandaa timu yakukutana na Marumo iliyofika nusu fainali na si timu inayofanya vibaya katika ligi ya nchini kwao.
“Marumo ni timu nzuri na sisi tunajiandaa kucheza na timu iliyofika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na sio nafasi yao kwenye msimamo wa Ligi (PSL) ya kwao Afrika Kusini.” Nasradinne Nabi.
Nae mlinda mlango Metacha Mnata akiongea kwa niaba ya wachezaji amesema “Kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo wa kesho, tunahitaji kuwa sehemu ya historia kubwa kwa klabu. Tunaomba sapoti yenu mashabiki twende tukashinde pamoja.”
Katika hatua nyingine Marumo Gallants wamegomea kupanda basi lililoandaliwa na wenyeji wap Yanga walipotua Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalim Nyerere majira ya saa tisa alfajiri.
Yanga waliwaandalia basi kubwa wageni wao lakini wao walilikataa na kupanda basi dogo waliloliandaa wenyewe ambalo liliwafwata uwanjani hapo na kuondoka nalo kuelekea hoteli waliyofikia.