Msimu wa ligi hapa nchini unarudi tena baada ya kusimama kutokana na janga la Covid-19 ambalo liliikumba dunia kwa kiasi kikubwa na kusababisha shughuli mbalimbali zisimame zikiwemo shughuli za michezo.
Serikali ya Tanzania imeshatangaza rasmi kuanzia jana tarehe 1/06/2020 kuwa ligi mbalimbali zinaweza zikaanza , na bodi ya ligi imeshatangaza rasmi urejeo wa ligi kuu Tanzania bara pamoja na kombe la shirikisho.
Timu mbalimbali zimeshaanza mazoezi ya kujiandaa na urejeo mpya wa ligi hapa nchini , Simba Sc wamekuwa wakitumia uwanja wao wa mazoezi wa Mo-Simba Arena uliopo Bunju kwa ajili ya kufanya mazoezi.
Yanga nao wamekuwa wakitumia uwanja wa Law School kwa ajili ya kufanya mazoezi yao kujiandaa na ligi kuu pamoja na kombe la shirikisho hapa nchini Tanzania.
Wakati Yanga na Simba wakiwa wanaendelea na mazoezi yao , klabu ya Azam FC wao walikuwa wanaendelea na mazoezi bila ya kocha wao mkuu , Aristica Cioba.
Lakini kwa mujibu wa Afisa habari wa Azam FC , Zaka Za Kazi amedai kuwa kesho kocha huyo ataungana na timu kwenye uwanja wa mazoezi wa Azam Complex.
“Kocha mkuu wa Azam FC ataungana na vijana kuanzia kesho kwenye mazoezi ya timu ambayo yanafanyika kwenye uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi”- alisema Zaka za kazi.
Kuhusu wachezaji wa kigeni waliopo makwao kwa muda huu , Zaka za Kazi amedai kuwa Azam FC unajitahidi kadri ya uwezo wao ili kuhakikisha hao wachezaji wanakuja mapema.
“Tunawasiliana na Ghana , Ghana nchi yao imeanza kulegeza masharti, vyuo vimeanza kufunguliwa ingawa bado hawajafungulia mipaka . Zimbabwe washafungulia mipaka tunatazama namna gani wachezaji wetu wanaweza kuja mapema kutoka Zimbabwe. Uganda bado hawajafungulia nchi”- alimalizia Afisa habari huyo.