Miongoni mwa nyota wanaotegemewa ndani ya kikosi cha Simba ni Mzambia Clatous Chama na kuelelea mchezo wa robo fainali dhdi ya Wydad Casablanca amebeba matumaini ya benchi la ufundi katika kuivusha timu hiyo katika mchezo huo wapili.
Baada ya kupata ushindi wa bao moja bila katika mchezo wa kwanza sasa Simba wanapaswa kuulinda ushindi huo ili kuweza kufuzu nusu fainali dhidi ya mabingwa watetezi Wydad Casablanca katika dimba la Mohamed V.
Kuelekea mchezo huo kocha wa Simba Robertinho Oliveira amesema “Itakua mechi tofauti kwasababu tunacheza nje ya Tanzania. Tumejaribu mbinu mbili ndani ya wiki hii na leo jioni kwa kushirikiana na wenzangu tutaamua mbinu ya kutumia kwenye mchezo huu. Naamini katika vipaji walivyonavyo wachezaji wetu.”
Nae kiungo wa pembeni wa Simba Pape Osmane Sakho akiongea kwa niaba ya wachezaji wa Simba amesema wao kama wachezaji wapo tayari kupambana ili kutimiza ndoto yakufuzu nusu fainali.
“Tupo tayari kupambana, tumejituma sana hadi kufikia hatua hii hivyo tutaendelea kujituma ili tuweze kufuzu nusu fainali,” alisema Sakho
Kuelekea mchezo huo Simba watamkosa Aishi Manula pekee huku wachezaji wengine wote wakiwa fiti kuweza kutumika dhidi ya Wydad Casablanca katika mchezo utakaopigwa saa moja usiku kwa saa za Morocco wakati kwa Tanzania itakua ni saa tatu usiku.