Kipigo cha mabao mawili kwa sifuri walichokipata KMC mbele ya Geita Gold katika Uwanja wao wa nyumbani Uhuru kimezidi kuwaweka katika hali mbaya “Kino Boys” katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
KMC imekubali kichapo hicho mbele ya ‘Wachimba dhahabu hao na kuwafanya kubaki na alama zao 26 wakiwa nafasi ya 4 yaani timu ya tatu kutoka mkiani wakati Geita wao wamefikisha alama 37 na kupaa mpaka nafasi ya tano.
Akizungumzia mchezo wa leo kocha mkuu wa KMC Hitimana Thiery amesema mchezo wa leo wameupoteza wenyewe kutokana na kufungwa goli la mapema lililowatoa mchezoni.
Hitimana Thiery ” Kweli tulikuja na plan nzuri, tulianza kucheza lakini nafikiri mwanzo haukua mzuri. Tuliruhusu goli katika dakika ya pili goli ambalo lilikua la mbali tu, kila mtu alikua nafasi yake ni mpira uliopigwa wakushtukiza nafkiri kipa alisimama vibaya na bahati mbaya mpira ukaingia golini,” alisema na kuongeza
“Hiyo ndio ilitutoa kwenye mchezo kwasababu wao kama Geita hawana cha kupoteza, walikua wanashambulia kwa kushtukiza na kubaki nyuma na hapo sisi tukatoka mchezoni na kupata stress kutokana na nafasi yetu tulipo chini.”
Akizungumzia uwezekano wa timu yake kushuka daraja Hitimana amesema Ligi ni ngumu lakini hawana namna njia pekee ya kubaki Ligi kuu ni kushinda michezo iliyopo mbele yao.
“Naamini misimu yote haipo sawa na haifanani, huu ni msimu mgumu sana nikiwa na KMC na ni msimu mgumu nikiwa kama kocha.
Nafasi tuliyopo ni ngumu na tutafanya juhudi zote ili tuweze kusogea juu, hakuna namna ni lazima tucheze na tushinde mechi tusogee juu zaidi ya hapa tulipo,” alisema Hitimana Thiery.