Klabu ya KMC FC leo imepokea basi jipya lenye thamani ya shilingi milioni 450 ambalo limetolewa na Benki ya NBC kwa makubaliano ya mkopo wa mwaka mmoja kwa lengo la kurahisisha usafiri kwa wachezaji.
Basi hilo limekabidhiwa mbele ya Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amosi Makala, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambuli, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge, Mkurugenzi Hanifa Suleiman Hamza pamoja na Makamu Mwenyekiti wa KMC FC Mhe. Rehema Mandingo.
Akizungumza wakati wa kukabizi gari hilo la kisasa linaloweza kubeba watu 58 Mhe. Makala ameipongeza Timu ya KMC FC kwakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba inawajali wachezaji wake na hivyo kuwapatia huduma nzuri ya usafiri.
” Niwapongeze sana KMC FC kwakuona fursa hiii kutoka Benki ya NBC ambao ni wazamini wakuu wa Ligi yetu, Timu nyingine ziige na kuacha visingizo vya magari kuwa yapo gereji, KMC FC imeonesha ukubwa wao na mazingatio ya malengo waliyokuwa nayo,” alisema Amos Makala
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambuli amesema “Tunafahamu wote faida ya michezo, leo tumepokea basi hili na hivyo ninampongeza Mkurugenzi, Meya kwa kufanikisha hili na hivyo kupunguza gharama ya uendeshaji wa usafirishaji wa timu.”
Mtambuli ameishukuru pia Banki ya NBC kwakujitoa kwenye ligi lakini pia kushuka hadi kwenye Timu ya KMC FC kwa kukubali kutoa gari wenye mkopo nafuu na kuahidi kulitunza ili liweze kutumika vizuri sambamba na kusimamia mkopo huo ili uweze kurudi kwa wakati na hivyo kuendelea kuwekeza zaidi katika sekta hiyo muhimu ya michezo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya , Mhe. Songoro akipokea basi hilo amesema kuwa kama Manispaa ya Kinondoni imejipanga kwa kuweka kwenye bajeti malipo ya mkopo huo kwa kipindi cha mwaka mmoja na kufanikisha kwa ufanisi mkubwa.
Mhe. Songoro amesisitiza kuwa KMC FC ndio Timu pekee kubwa ambayo ipo kwenye ligi kwa ajili ya kuleta mapinduzi makubwa katika Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania kutokana na kujipanga vema katika nyanja mbalimbali.