Wana “Kino Boys” KMC FC wamesema licha ya kuwa katika nafasi mbaya katika msimamo wa Ligi lakini bado nafasi wanayo na watapambana kuhakikisha wanabaki Ligi Kuu msimu ujao.
KMC mpaka sasa wanashika nafasi ya 13 wakiwa na alama 29 baada ya kushuka dimbani mara 28. Akizungumza na tovitu ya Kandanda.co.tz msemaji wa KMC Fc Christina Mwagala ametoa taarifa ya kikosi na kuweka wazi malengo yao kuelekea michezo miwili iliyobaki.
“Kikosi kimeingia kambini leo Jumatatu kwa maandalizi kuelekea michezo miwili yakwenda kumaliza Ligi msimu wa 2022/2023 ambapo tutakua ugenini dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City. Mchezo dhidi ya Prisons tutacheza Sokoine Mbeya wakati ule wa Mbeya City utachezwa Nelson Mandela Rukwa,” alisema Mwagala
Wachezaji wa KMC chini ya kocha Jamhuri Kihwelo Julio tayari wamesharudi kambini wakiendelea kujifua baada ya likizo ya siku mbili waliyoipata kufuatia ushindi dhidi ya Singida Big Stars
“Wachezaji wote wamerudi salama baada ya kumaliza mchezo wetu dhidi ya Singida Big Stars ambao tulipata ushindi wa mabao mawili. Tulitoa mapumziko ya siku mbili Jumamosi na Jumapili, leo hii Jumatatu asubuhi tumeanza maandalizi. Tunakwenda katika michezo ambayo ni migumu na ukizingatia hatupo katika nafasi nzuri (tupo katika nafasi ya 13) sio sehemu salama kwetu,” alisema na kuongeza
“Nitoe rai kwa mashabiki wote wa KMC na wakazi wa Kinondoni kwamba bado tuna nafasi yakwenda kupambana mpaka tone la mwisho, ni kipindi ambacho tunahitaji kutumika zaidi ili msimu unaokuja tuweze kuwepo. Tunahitaji msimu ujao tuweze kuwepo ili tuweze kutumia basi letu jipya lakisasa kabisa lakini pia tuweze kutumia uwanja wetu mpya “Old Traford ya KMC” uliopo pale Mwenge.”
KMC ilinunua basi jipya na lakisasa mapema mwaka huu kwa ushirikiano na benki ya NBC na hivyo kuwa miongoni mwa vilabu vyenye mabasi mazuri kabisa nchini. Lakini pia wapo katika ujenzi wa uwanja wao wa nyumbani unaojengwa katika eneo la Mwenge ambapo ukikamilika utakua ni uwanja wapili katika Wilaya ya Kinondoni wakiungana na ule wa Mbweni JKT unaotumiwa na JKT Tanzania.