Timua ya KMC “KINO BOYS” walisafiri kuelekea mkoani Rukwa ambako watacheza michezo wao wa Ligi dhidi ya Tanzania Prisons na kwenda Mbeya kucheza dhidi ya Mbeya city.
Akizungumza na tovuti ya kandanda.co.tz Christina Mwagala afisa habari wa KMC Fc ameongelea kuhusu safari yao ilivyokuwa kuelekea mkoani Rukwa.
“Tumefika salama Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo tutakuwa hapa kwa kipindi cha siku kumi ikiwa ni katika sehemu ya kumalizia mechi zetu mbili za ligi kuu ya NBC, tarehe 6 ya mwezi huu wa sita tutakuwa ugenini dhidi ya Tanzania Prisons na tarehe 9 ya mwezi wa sita tutakua pia ugenini dhidi ya Mbeya City, kikubwa tunamshukuru mwenyezi mungu safari ilikua nzuri hakukuwa na changamoto yoyote.”
Hakuishia hapo afisa habari huyo aliieleza kandanda.co.tz kuhusu hali za wachezaji na benchi la ufundi, mikakati yao pamoja na maandalizi kuelekea michezo hii muhimu.
“Wachezaji wamefika salama wakiwa na afya njema wana hali na morali na ukizingatia kwamba maandalizi yetu tulishayafanya tangia tukiwa Dar es salaam kwasababu michezo hii ilikuwa kwenye ratiba kwamba tutakwenda kumaliza mechi zetu mbili ugenini, kwa maandalizi yamekwenda vizuri na kwamba huku Sumbawanga kuna hali ya baridi sana tofauti na Dar es salaam, tutakua na programu mbalimbali ambazo zitasaidia kuwaweka wachezaji vizuri lakini pia kuendana na mazingira ambayo ni tofauti na yale tuliyoyazoea kule Dar es salaam,” alisema Mwagala.
Mkurugenzi wa KMC Khanifa Suleiman Hamza na viongozi wengine wa timu hiyo hawako nyuma, wanapambana na kuhakiksha timu yao inabaki na kuendelea kucheza ligi kuu NBC msimu ujao.
“Viongozi wametupa baraka zote na kutuelekeza kwamba tuje tupambane kufa kupona ili kuhakikisha Manispaa yetu ya Kinondoni inasalia kwenye ramani na kuendelea kutoa ushindani katika ligi kuu Tanzania bara na michuano mingine,” alisema na kuongeza “Tunawaahidi, tunakuja kwenye mechi ngumu sana na mechi za huku sio nyepesi kama ambavyo mechi nyingine tumetoka kucheza lakini tutakwenda kupambana tutafia uwanjani.”
“Tutazimia uwanjani, tutalala uwanjani, ilimradi tuhakikishe Manispaa ya Kinondoni inaendelea kuwepo kwenye ramani ya Ligi kuu msimu unaokuja, asanteni” msemaji huyo alimaliza.
KMC akifanikiwa kushinda michezo hiyo miwili iliyosalia itajihakikishia nafasi ya kuendelea kuwepo katika Ligi kuu ya NBC msimu ujao. Je Prisons na Mbeya city wako tayari kufanywa ngazi ya wao kubakia Ligi kuu? Kipi kitatokea kama mambo yatakwenda tofauti? Tusubiri na kuona.