Sambaza....

Mzunguko wa pili wa Ligi kuu ya NBC soka Tanzania bara unaendelea kesho ambapo Timu ya KMC FC itawakaribisha Coastal Union ya mkoani Tanga katika Uwanja wa Uhuru hapa Jijini Dar es salaam mchezo utakaopigwa saa 16:00 jioni.

KMC FC chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana imekamilisha maandalizi ya mchezo huo na kwamba wachezaji wote wapo tayari kuanza vema mzunguko wa pili kwa kuhakikisha kwamba inafanya viziri katika michezo yote licha ya ushindani uliopo.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana ambayo ipo katika nafasi ya 10 mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC na alama 16 imejihakikishia kupambana katika mzunguko huo wa pili kwa kuwa ni hatua ya kuelekea kumalizika kwa msimu wa 2022/ 2023.

Akizungumzia kuanza kwa mzunguko huo wa pili hapo kesho, Hitimana amesema kuwa kama Timu imejipanga vizuri kutokana na kwamba michezo ya mwisho haikuwa na matokeo mazuri na hivyo changamoto kubwa ilitokana na wachezaji wengi kuwa na majeraha lakini kwasasa wanne wamerejea jambo ambalo limeleta matumaini makubwa.

Mashabiki wa KMC

” Tunafahamu kuwa mzunguko wa pili utakuwa na ushindani zaidi kutokana na kwamba kila Timu inahitaji kufanya vizuri na hivyo tunakwenda kupambana ili tupate matokeo mazuri kwakuwa michezo yote ipo ndani ya uwezo wetu.

Kuhusu mchezo wa kesho Hitimana amesema kuwa KMC FC itawakosa wachezaji wawili ambao ni Hance Masoud pamoja na Emmanuel Mvuyekure kutokana na chamgamoto za majeraha na kwamba wengine wapo kwenye hari na morali nzuri hivyo kila mmoja yupo tayari kutumika kwa ajili kupata alama tatu.

“Coastal Union ni Timu nzuri hata ukiangalia katika mchezo wao wa mwisho walipata ushindi wakiwa ugenini, lakini hatuliangalii hilo kama changamoto badala yake tunajiandaa kwa ajili kuhakikisha kuwa tunatumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani hapo kesho.


Sambaza....