Klabu ya KMC FC inakabiliwa na changamoto ya wachezaji sita tegemeo ambao ni majeruhi ndani ya kikosi hicho ambapo kwasasa wanaendelea na matibabu.
Wachezaji hao ni Hance Masound ambaye aliumia jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Singida Big stars na hivyo kushindwa kuendelea jambo lililopelekea kukimbizwa Hospitali na gari la wagonjwa (Ambulence).
Wachezaji wangine ambao jana walishindwa kuendelea na mchezo mbali na Hance Masound ni Ibrahim Ame, Baraka Majogoro ambao pia kwa nyakati tofauti katika mchezo huo uliomalizika kwa KMC FC kupoteza kwa bao moja ugenini walishindwa kuendelea na mchezo kutokana na kupata majeraha.
Aidha wachezaji wengine ni Kelvin Kijili, Awesu Ally Awesu pamoja na Emmanuel Mvuyekure ambao hawa pia walikuwa na majeraha ya muda mrefu hali iliyopelekea kushindwa kusafiri na Timu kwenye mchezo dhidi ya Singida big Stars.
“Kwasasa tunakabiliwa na changamoto kubwa ya wachezaji wenye majeraha, na ukiangalia kwenye Timu kila mchezaji anamchango mkubwa pindi anapopewa majukumu na kocha, hivyo nikipindi kigumu lakini tutajitahidi kadiri tuwesavyo ili kufanya vizuri kwenye michezo inayokuja.” Christina Mwagala afisa habari wa KMC
Katika hatua nyingine KMC FC imerejea Jijini Dar es salaam alfajiri ya leo ikitokea mkoani Singida na kwamba kesho itaanza kufanya maandalizi kuelekea katika mchezo unaokuja dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Novemba 28 katika uwanja wa Uhuru Jijini hapa.