Sambaza....

Klabu ya soka ya Alliance fc ya jijini Mwanza ni kama imezinduka hivi kutoka usingizini baada ya kufanya vyema katika michezo yao ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Bara na kupelekea kufufua matumaini ya kubaki Ligi Kuu.

Katika michezo mitano ya hivi karibuni Alliance Fc wamefanikiwa kukusanya alama 11 kati ya 15. Alliance mara ya mwisho kupokea kipigo ilikua ni katika mchezo dhidi ya KMC ugenini kwa mabao mawili kwa moja.

Luseke Geofrey na Hussein Omary walishangilia.

Alliance pia imeondolewa katika robo fainali ya kombe la FA na Namungo fc kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri. Wamefanikiwa kufika hatua hiyo mara tatu mfululizo lakini wamejikuta wakishindwa kuendelea mbele na kutolewa hatua hiyo.

Tovuti ya Kandanda imefanikiwa kuongea na kiungo David Richard Ulomi ili kufahamu ni kipi kipo nyuma ya mwenendo huu mzuri wa klabu kuelekea mwishoni mwa msimu.

David Ulomi akimuacha mlinzi wa Mtibwa Sugar  Dickson Job katika uwanja wa Nyamagana.

Ulomi David “Tulipata muda mrefu wakufanyia kazi mapungufu yetu tuliyokuwa nayo na sisi kama wachezaji tulikuwa hatufurahishwi na matokeo tuliyokuwa tunapata kwaiyo tukaamua tufanya mazoezi kwa juhudi zaidi”

Kiungo huyo mwenye mabao saba na pasi nne za mabao hakuishia hapo tuu lakini aliweka wazi malengo yao waliyojiwekea kipindi hiki Ligi ikiwa imebakisha michezo minne pekee.

Ulomi wa Alliance fc akitafuta namna ya kumuacha mchezaji wa Lipuli fc.

“Tunataka kupambana tumalize nafasi nzuri na hatutakubali kushuka daraja, tupo chini lakini tunasogea juu. Kwa hii michezo minne iliyobaki tutapambana kuhakikisha Chama halishuki daraja.” Ulomi.

Mpaka sasa Alliance fc inashika nafasi ya 14 wakiwa na alama 40 huku wakiwa wameshuka dimbani mara 34. Alliance wamebakiwa na michezo minne pekee ili kumaliza Ligi Kuu Bara.

Sambaza....