Sambaza....

Uongozi wa klabu ya soka ya Stand United umelitaka Shirikisho la Kandanda nchini kupitia Bodi ya ligi kuwapatia alama tatu baada ya Alliance kumtumia Bigirimana Blaise kwenye mchezo wao wa ligi siku ya Ijumaa wakati akiwa bado na mkataba na wapiga debe hao.

Mwenyekiti Stand United Ellyson Maeja amesema Alliance wamevunja kanuni kwa maksudi wakijua kuwa Blaise sio mchezaji wao lakini wakamtumia katika mchezo huo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na kuisha kwa sare ya bao 1-1.

“Nataka ufafanuzi kutoka bodi ya ligi ni kwa vipi mchezaji anaruhusiwa kucheza akiwa kwenye pingamizi, unajua kabla ya mchezo nilimuona Blaise akifanya mazoezi nikampigia Baraka Kizuguto akasema huyo mchezaji ana leseni, nikahoji leseni anatoa wapi wakati sisi hatujampa Release Letter?

“Sisi hatujawahi kuona kitu kama hicho, mchezaji kucheza akiwa na malalamiko, hatujawahi kumpa barua ya kumruhusu, hatujaingia kwenye mtandao na kuruhusu acheze, tulikataa, bado ni mchezaji wetu bado anamiezi sita ya mkataba, hata ukiangalia kwenye mfumo ni mchezaji wa Stand United,” Maeja amesema.

Kwa upande wake msemaji wa Alliance amesema hajawafanya makosa kumtumia Bigirimana Blaise katika mchezo huo kwani tayari ni mchezaji wao halali baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili.

“Bigirimana ni Professional anafahamu haki zake, anafahamu wazi kwamba Stand United wamevunja mkataba wake, pia sisi ni wasomi kila tunachofanya tunafanya kwa utaratibu, tuliongea na meneja wake na kufanya taratibu za kumsajili, siku hizi ukimsajili mchezaji kama anamkataba na timu nyingine huwezi kufanikiwa maana majina yapo kwenye mtandao, sasa sisi jina lake limesoma na tumepata leseni,” Mwafulango amesema.

Sambaza....