Kuna taarifa kocha mkuu wa Azam Fc, mwalimu Hans Van Der Pluijm na msaidizi wake Juma Mwambusi wamefukuzwa kazi na timu ya Azam Fc.
Baada ya taarifa hizi kuzagaa kuna taarifa zingine zinaendelea kuzagaa kama tetesi za makocha ambao wanapewa nafasi ya kuziba nafasi za Mholanzi huyo.
Kuna makocha watatu ambao wameonekana kutajwa sana kuja kuchukua nafasi ya mwalimu Hans. Kocha wa KMC, Ettiene Ndaragije anatajwa kwenye tetesi hizi, Masoud Djuma aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Simba anatajwa pia.
Lakini tetesi kubwa ni jina la Mwinyi Zahera kuibuka kama kinara kwenye orodha ya makocha wanaotakiwa na Azam Fc. Sasa kama Mwinyi Zahera ataenda Azam Fc kipindi hiki mambo yapi yatatokea ?
KUDHOOFIKA KWA YANGA KWENYE MBIO ZA UBINGWA.
Moja ya vitu ambavyo Yanga wanatakiwa kuviweka katika maombi yao ni Mwinyi Zahera kutoondoka kipindi hiki.
Kipindi ambacho timu iko kwenye sura ya kugombania ubingwa. Na sehemu hiyo ya kugombania ubingwa wa ligi kuu mtu pekee ambaye ameiweka ni Mwinyi Zahera.
Pamoja na kwamba Yanga wapo katika mazingira ambayo ni magumu kiuchumi lakini Mwinyi Zahera amefanikiwa kuwajenga wachezaji wa Yanga kisaikolojia.
Wanapigana vizuri bila kujalisha hali mbaya ya uchumi iliyopo ndani ya klabu. Na ndiyo sababu kuu ambayo imepelekea Yanga mpaka sasa kuwepo kileleni mwa ligi kuu Tanzania bara.
Sasa akiondoka kipindi hiki ambacho ligi inaendelea kutakuwa na nafasi kubwa sana kwa Yanga kudhoofika katika mbio za ubingwa.
Kwa sababu itachukua tena muda mrefu kwa Yanga kumpata kocha ambaye anaweza kupigana na wachezaji katika hali hii mbaya ya kiuchumi. Yani kuwafanya wachezaji wapigane bila kujali hali mbaya ya kiuchumi.
Tuliona msimu jana , mwalimu George Lwandamina alifanikiwa kuwajenga vizuri wachezaji lakini alipoondoka tu , timu ilidhoofika sana.
Kwa hiyo Yanga wanachotakiwa ni kuhakikisha mwalimu Mwinyi Zahera kubaki katika kikosi chao mpaka pale msimu huu utakapomalizika.
MABADILIKO YA KIMFUMO KWA AZAM.
Kocha Hans Van Der Pluijm alikuwa akitumia mfumo wa 4-4-2 kwenye karatasi, ingawa kiuhalisia alikuwa anatumia 4-2-3-1 akiwa uwanjani, na kuna wakati timu ilikuwa inarudi kwenye umbo lake la 4-4-2 .
Lakini Mwinyi Zahera akiwa na Yanga amekuwa akitumia mifumo mbalimbali, kama 4-4-2 Diamond Shape, ambapo wachezaji ambao huonekana kwenye karatasi kucheza pembeni wao hushuka katikati mwa uwanja kujaza idadi ya viungo.
Pia Mwinyi Zahera amekuwa akitumia mfumo wa 4-3-3 akiwa na Yanga. Kwa hiyo kama Mwinyi Zahera ataenda katika timu ya Azam Fc kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kimfumo ndani ya timu ya Azam Fc.
USHIRIKIANO NA VIONGOZI
Moja ya malalamiko ambayo Mwinyi Zahera aliwahi kulalamika ni yeye kutosikilizwa na viongozi wa Yanga katika mambo ya usajili.
Ambapo alipendekeza baadhi ya wachezaji katika dirisha dogo lakini viongozi wakashindwa kumtimizia.
Azam Fc wamekuwa na utamaduni wa kuwasikiliza makocha wao linapokuja suala la usajili.
Tumemuona mwalimu Hans ambavyo amepewa nafasi ya kuwasijili wachezaji aliowapendekeza kama Kutinyu, Chirwa.
BAADA YA KUPEWA NAFASI YA USAJILI, AZAM FC INAWEZA KUWA TIMU IMARA
Kama kocha Mwinyi Zahera atapewa nafasi ya kusikilizwa yeye kama kocha aina ya wachezaji ambao anawahitaji basi kuna uwezekano mkubwa kwa Azam Fc kurudi kuwa timu imara.
Kocha wa mwisho kuipa ubingwa Azam Fc ni kocha Joseph Omong baada ya hapo hakuna kocha ambaye aliwahi kuipa ubingwa Azam Fc kwa hiyo kuna nafasi kubwa sana kwa Mwinyi Zahera kupata nafasi ya kuipa ubingwa Azam Fc kama akipewa mazingira bora.
ATAWEZA KUFANYA KAZI TIMU MOJA NA BENO KAKOLANYA ?
Kama ambavyo zilivyo tetesi za Mwinyi Zahera kutakiwa na Azam Fc ndivo hivo tetesi za Beno Kakolanya kutakiwa na Azam Fc.
Razack Abalora amekuwa na kiwango dhaifu Siku za hivi karibuni , na kuna taarifa Beno Kakolanya kuja kuchukua nafasi yake.
Tukumbuke Beno Kakolanya aliwahi kufanya kazi na Mwinyi Zahera na wakashindwa kuelewana, hivo swali kubwa linabaki kama wote wakienda Azam Fc wataweza kufanya kazi kwa pamoja ?