Sikukuu ya soka nchini imemalizika , Simba ndiyo wamepata nafasi kubwa ya kusherehekea vizuri sikukuu hii.
Kipi kimesababisha YANGA kufungwa ?
Moja ya sababu kubwa ambayo imempa nafasi kubwa Zana Coulibaly kung’ara leo ni jinsi eneo la kushoto la Yanga lilivyokuwa linatengeneza uwazi katika eneo lake.
Hii ilikuwa inasababishwa na vitu viwili, cha kwanza Gadiel Michael kuwa anasimama juu muda mwingi na kufanya uwazi katika eneo lake.
Cha pili ni namna ambavyo Yanga ilikuwa haina mchezaji wa pembeni kwa upande wa Ushambuliaji.
Mchezaji ambaye angekuwa na uwezo wa kushuka kuja kumsaidia Gadiel Michael kukaba, ndiyo maana Zana Coulibay na Emmanuel Okwi walimtesa sana Gadiel Michael.
Kama ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza ambavyo upande wa kushoto wa Yanga ulivyokuwa unatengeneza uwazi ndivyo hivo goli la Simba lilivyopatikana.
Gadiel Michael alikuwa amepanda juu kama ambavyo alikuwa anafanya kipindi cha kwanza na kuchelewa kurudi nyuma kukaba.
Alipokuwa amepanda juu kitu ambacho kilisababisha kuwa na uwazi kwenye eneo la nyuma la Yanga. Uwazi ambao aliutumia John Bocco kujipenyeza na kupiga krosi kwa Meddie Kagere aliyefunga goli.
Kwanini leo Chama kafichwa?
Leo Yanga walijaza viungo halisi wa kati watatu (Abdalah Shaibu Ninja, Feisal Salum “Fei Toto” na Papy Kabamba Tshishimbi.
Pamoja na kwamba walikuwa na viungo watatu, pia wachezaji wengi wa Yanga walikuwa wanashuka katikati kuongeza idadi ya viungo wa Yanga.
Mfano, Ibrahim Ajib alikuwa anashuka katikati ya uwanja na kuongeza idadi ya viungo wa Yanga kuwa wanne dhidi ya watatu wa Simba.
Hali ambayo ilikuwa virahisi kwa Yanga kuwabana Simba katika eneo la kiungo. Hivo mchezaji kama Chama kuonekana kupwaya.
Pamoja na kwamba Chama amepwaya kwenye mechi hii pia hata viungo kama James Kotei na Jonas Mkude walikuwa hawana uwezo wa kupanda juu.
Tumezoea kwenye baadhi ya mechi nyingi James Kotei na Jonas Mkude huwa wanachezea juu sana kuisukuma timu yao Iwe juu.
Lakini hii ilikuwa tofauti leo kwa sababu Yanga ilikuwa na idadi kubwa ya watu eneo hili. Hali ambayo iliwafanya kina James Kotei na Jonas Mkude kutokuwa na nafasi ya wao kusogea mbele kuisukuma timu.
Kipi kimesababisha Yanga kutokupata goli?
Aina ya washambaliaji walianzishwa leo na Mwinyi Zahera ( Amis Tambwe na Makambo) mara nyingi huwa mashujaa sana kwenye mipira ya kichwa.
Je walipangiwa wachezaji sahihi kulingana na aina ya uchezaji wao ?
Jibu hapa ni hapana. Leo Yanga walitakiwa kucheza na washambuliaji wa pembeni ambao wangekuwa na uwezo mkubwa wa kupiga mipira ya krosi.
Mwinyi Zahera aliamua kucheza 4-4-2, ambapo wachezaji wa pembeni walikuwa wanakuja katikati kuongeza idadi ya viungo na kuacha pembeni Iwe kazi ya mabeki wa pembeni (Paul Godfrey na Gadiel Michael) kupiga krosi.
Ilikuwa ngumu kwa Yanga kupita katikati ya uwanja kwa sababu eneo hili ni bora sana kwa Simba hivo isingewapa nafasi Yanga kufanya vyema kupitia katikati.