Meneja wa timu ya soka ya African Lyon, Adam Kipatacho amesema sare ya mchezo wao dhidi ya Alliance kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara uliofanyika CCM Kirumba ilipatikana baada ya lengo la kulilinda bao walilolipata kipindi cha kwanza kushindikana.
Kipatacho amesema sio kwamba walizidiwa katika mchezo hadi kuruhusu bao la kusawazisha lakini waliamua kucheza mchezo wa kujilinda kutokana na kwamba walikuja Mwanza kwa lengo la kupata walau sare wakijua fika kuwa Alliance ni timu nzuri.
Amesema lengo lao lilikuwa ni kupata sare, lakini walipopata bao kupitia kwa Haruna Moshi mipango yao ilibadilika na kuona kuwa wanaweza kulizuia bao hilo lakini hali ilikuwa tofauti kwani Mwamuzi aliamua kuwapa bao Alliance katika dakika za mwisho.
“Ukiangalia mchezo utaweza kusema kuwa tumezidiwa lakini hii ni 4-4-2 ambayo ilikuwa maalumu kwa ajili ya kujilinda zaidi kuliko kushambulia lakini hiyo hiyo tulipata bao, sisi huku tulikuja kuchukua pointi moja, lengo hasa lilikuwa hilo kama ilivyo Shinyanga pia tuchukue pointi moja halafu Kagera tukashinde turudi Dar es Salaam na pointi sita,”
“Kwa hiyo ndio maana mwalimu alipanga hivyo katika mfumo wa uchezaji, sio kwamba tulizidiwa, mwamuzi kaamua kuwapa goli sawa tumekubali matokeo, umeona kabisa pale kipa amepigwa mangumi, kasukumwa mpira unatakiwa uchezwe miguuni,” Kipatacho ameeleza.
Kwa sasa African Lyon wanajiandaa na safari ya kuelekea mkoani Kagera ambapo watakuwa na mchezo dhidi ya Wanankurukumbi Kagera Sugar katika uwanja wa Kaitaba Jumamosi ya Septemba mosi mwaka huu.