Wengi tulimshangaa kuona anaihama Arsenal na kwenda Liverpool. Macho yetu yalituonesha anatoka kwenye timu ambayo ana nafasi kubwa ya kupata nafasi na kwenda sehemu ambayo upatikanaji wa nafasi ulikuwa finyu kwa sababu kulikuwa na wachezaji ambao walionekana wana kiwango kikubwa zaidi yake.
Sehemu ya kiungo cha katikati alipokuwa anataka kucheza ndiyo sehemu ambayo ilikuwa imejaza watu ambao kwa haraka haraka ilionesha ni ngumu kwake yeye kuwakalisha kwenye mbao.
Hakujali na wala hakuona ugumu wowote kwenye hilo, alichokifanya ni kufuata matamanio yake yalipo, matamanio ambayo yalimuonesha anaweza kuwa mchezaji bora akiwa Liverpool na siyo Arsenal.
Sehemu ambayo alicheza kwa miaka 6 bila kuona maendeleo makubwa ya kipaji chake.
Umri ulikuwa unaenda kasi, na yeye alikuwa anataka mafanikio ,mafanikio ambayo yatatokana na kipaji chake .
Kipaji ambacho kilikuwa kinapoteza muda kukaa kwenye timu ya Arsenal, timu ambayo ilikuwa haina matanio makubwa ya ubingwa.
Matamanio ambayo yanaweza kusukuma jitihada za mchezaji binafsi ili apigane zaidi kwa ajili yake na kwa ajili ya timu.
Ndiyo maana Oxlaide Chamberlain ndani ya miaka 6 aliyokaa Arsenal na kucheza michezo 132 alifanikiwa kufunga magoli 9 tu , magoli ambayo ni robo ya magoli aliyoyafunga akiwa Liverpool kwenye nusu msimu.
Michezo 26 akiwa amefunga magoli 3 na kwenye michezo 10 zilizopita amefanikiwa kutoa pasi 5 za mwisho na kufunga goli 1.
Hivi vyote inaonesha kuwa kuna mabadiliko makubwa ndani yake, mabadiliko ambayo yamesababisha yeye afanye vizuri kipindi hiki ambacho yupo Liverpool kuliko ƙkipindi kile alichokuwepo Arsenal.
Hii ni kutokana na aina ya ƙkocha na timu ambayo yupo kwa sasa.
Timu na kocha wana nafasi kubwa sana katika kuleta mafanikio makubwa kwenye kipaji cha mchezaji husika.
Oxlaide Chamberlain alikuwa anakosa timu ambayo ilikuwa na kocha ambaye anataka mafanikio ya ndani ya uwanja.
Kocha ambaye kwake yeye ushindi wa timu ni kitu cha muhimu, kocha ambaye anaweza kuwalisha sumu wachezaji ili wapigane kwa ajili ya timu.
Kocha ambaye anaweza kumfanya mchezaji ajiamini, aamini kuwa ana kipaji kikubwa ndani yake.
Kocha ambaye haoni aibu kukuadhibu wa kukukalisha benchi siku ambayo umefanya vibaya ili kujipa muda wa kujitafakari na kujirekebisha.
Vitu vyote hivi havipo ndani ya kikosi cha Arsenal na wachezaji wengi wanakosa hivi vitu.
Wachezaji wa Arsenal hawajiamini , na hii kwa sababu kocha waliye naye hana uwezo wa kupandikiza mbegu za wao kujiamini.
Wachezaji wa Arsenal hawapigani mpaka mwisho kwa ajili ya kupata matokeo chanya hii ni kwa sababu kocha waliye naye hana uwezo wa kuwahamasisha kupigana mpaka sekunde ya mwisho.
Vitu hivi vyote Liverpool vinapatikana na kwa bahati nzuri Oxlaide Chamberlain amefanikiwa kuvipata.
Oxlaide Chamberlain wa sasa anajiamini , anapigana kwa ajili ya timu yake na kipaji chake na hii ni kwa sababu Jurgen Klopp anafanya kazi kila siku kumfanya awe bora.
Na hii ni kuonesha kuwa kocha ana nafasi kubwa sana katika ƙmaendeleo ya kipaji cha mchezaji wake.
Arsene Wenger aliwahi kuwa mzuri sana katika kukuza , kulea na kuvifanya vipaji vya wachezaji mbalimbali kung’ara.
Lakini muda huu hana tena uwezo huo, nguvu zimepungua katika akili yake, mwili wake umechoka hana tena huo uwezo.
Uwezo wa kumfanya mchezaji apigane kwa ajili ya timu, mchezaji ajiamini. Mechi mbili dhidi ya Manchester City, wachezaji walikuwa hawajiamini tofaufi na wachezaji wa Manchester City.
Kuna wakati ilikuwa ngumu kwao kupigana kwa ajili ya kufunga hata goli moja ambalo lingewarudisha mchezoni kwa sababu hawakuwa na mtu kwenye benchi la ufundi ambaye angeweza kuwafanya wapigane na kupambana kwa nguvu ili kurudi mchezoni
Nyuso zao zilikuwa zinaonesha hawana uwezo wa kufanya kitu chochote kikubwa ndani yao.