Katibu mkuu wa klabu ya soka ya Mwadui ya mkoani Shinyanga Ramadhan Kilao amesema wamejiandaa vyema kuelekea katika mchezo wao wa tatu wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Azam FC na kwamba safari hii watahakikisha wanapata pointi zote tatu.
Akizungumza na mtandao huu Kilao amesema katika michezo miwili ya mwanzo ambayo wamecheza ugenini walishindwa kupata walau pointi moja na tayari wameshatambua tatizo lilipokuwa na kwamba tayari wameshalirekebisha.
Kilao amesema wameshafanya mazoezi kiasi cha kutosha katika kipindi hiki cha wiki moja na nusu ambapo ligi ilisimama kupisha majukumu ya timu ya Taifa, na imani yao ya kupata pointi tatu ni kubwa licha ya kwamba wanakwenda kukutana na timu ngumu ya Azam.
“Tumejiandaa, tumefanya mazoezi kiasi cha kutosha, na sasa hivi tunafanya mazoezi mepesi ili kwa ajili ya kusubiri mchezo wa Ijumaa ambao bahati mbaya utachezwa saa nane mchana, tumecheza michezo miwili tumepoteza Kagera na Singida kwa hiyo huu ni mchezo wetu wa kwanza kucheza nyumbani na nafikiri tunajiandaa kuutendea haki,” Kilao amesema.
Mpaka sasa Mwadui ni miongoni mwa mbili ambazo mpaka sasa hazijafanikiwa kupata hata pointi moja tangu ligi kuu ianze mwishoni mwa mwezi uliopita, timu nyingine ni Mbeya City ambayo yenyewe imecheza mechi tatu ikifungwa zote.