KUNA mambo yanashangaza sana katika soka la Tanzania. Mojawapo kati ya mambo hayo ni ili la Shirikisho la mpira nchini-TFF kutangaza hadharani kuwa michezo ya katikati ya wiki hii inayohusisha klabu za Yanga SC na Simba SC kusogezwa mbele ili kuzipa nafasi ya kujiandaa zaidi (inavyoaminika) klabu hizo kubwa zinazotaraji kuchuana katika ‘Dar es Salaam-Pacha’ Jumapili ijayo.
Kila mwanasoka nchini anafahamu kuhusu ukubwa wa klabu hizi, hata kama wapo watakaosema hapana, lakini historia inaonyesha hivyo na mataji 27 ya Yanga katika ligi, 19 ya Simba na vikombe vingine 11 vya Cecafa Kagame Cup walivyotwaa wabababe hao wa soka la Tanzania vinadhihirisha ukubwa wao.
Yanga ilianzishwa mwaka 1935 na Simba ikafuata mwaka mmoja baadae, hii inamaanisha klabu hizi ni kongwe pia ukiachana na ukubwa wao. Kataa, ukubali, huo ndiyo ukweli. Shirikisho la soka nchini ambalo kimsingi linaongozwa na wanachama wa klabu hizi kubwa linapaswa kutafuta njia nyingine ya kuzipendelea klabu hizi ili kuleta usawa katika ligi yenye timu 20.
Wakati ratiba inapangwa-wapangaji hao walifahamu kabisa kuwa timu ya Taifa ya Tanzania ina kawaida ya kuingia kambini walau siku saba hadi kumi kabla ya mchezo husika, pia kama wanafahamu kuwa Yanga na Simba zinapaswa kujiandaa zaidi kabla ya mchezo baina yao ni wazi wangeamua katika ratiba yao kila msimu klabu hizo kukutana katika mchezo wa ufunguzi kwa sababu tayari zinakuwa zimetoka katika maandalizu.
Ni aibu kubwa na muendelezo wa kufeli kwa utawala wa Wallace Karia ambaye aliingia madarakani mwaka mmoja uliopita. Tunaona kwa nchini za wenzetu zilizoendelea, kuna wakati Real Madrid na FC Barcelona zilikutana mara nne ndani ya siku 16 lakini hakukuwa na mabadiliko ya ratiba ili kuzipa klabu hizo kubwa za Hispania nafasi ya kujiandaa.
Real na Barca zilikutana katika nusu fainali ya Uefa Champions league msimu wa 2010/11, zikacheza fainali ya kombe la mfalme na mchezo wa marejeano wa La Liga ndani ya siku 16 tu, lakini kwa hapa Tanzania Simba na Yanga wanaenda kukutana kwa mara ya pili tu mwaka huu 2018 lakini maajabu kabisa TFF inasema mchezo wao unapaswa kuwa ‘maalumu’
Kuna wakati mtu unajiuliza na kushindwa kupata majibu yanayoweza kukutoa katika sintofahamu husika, je, ligi ya Tanzania ni mahususi kwa Yanga na Simba tu? Kama sivyo, Mtibwa Sugar v Kagera Sugar nao wakiomba muda wa kujiandaa kabla ya mchezo baina yao watakubaliwa licha ya kwamba Simba na Yanga hazikuomba zaidi ya ‘utashi’ tu wa watu wa TFF?
Nawaambia umoja kwa klabu unahitajika mno vinginevyo wataburuzwa hadi ‘kiama’. Sasa wanachezeshwa ligi ambayo hawajui wanashindania nini! Hii ni aibu pia lakini maajabu klabu hizi zenye viongozi wengi wanachama wa Simba na Yanga zinaendelea tu kucheza! Hizo ndiyo Simba na Yanga klabu ambazo mara zote nimekuwa nikisisita ni muhimu mno katika maendeleo ya soka la Tanzania. Zikifa na soka litakufa, zikipata mafanikio na timu ya Taifa inanyanyuka.
Nadhani tayari tumeingia katika ‘soka la kidikteta.’ Mkubali mkatae watakavyoamua TFF ndivyo itakavyokuwa hata kama klabu zinakuwa na haki ya kuhoji na kusikilizwa. Hilo ndiyo Shirikisho la soka nchini ambalo watendaji wake ni wanachama hai wa klabu za Simba na Yanga huku viongozi wengi wa klabu nyingine pia wakiwa ni watu wa Yanga na Simba hivyo si rahisi kupinga mambo kama haya yasiyovutia katika maendeleo ya soka.