Sambaza....

Miaka 88 imepita, miaka ambayo ilituonesha nchi 8 zikibeba kombe hili la dunia kwa nyakati tofauti, nchi ambazo zilikuwa na wachezaji nyota walioshiriki kuacha alama kubwa katika michuano.

Maisha ni alama, dunia itakukumbuka na kukuenzi kwa alama unazoziacha duniani wakati mwili wako ukiwa na nguvu na akili yako ikiwa na uwezo wa kufikiria ufanisi bora wa kazi unayoifanya ili uache alama kubwa duniani.

Magoli 2379 yamepatikana mpaka sasa kwenye michuano hii ya kombe la dunia ndani ya michezo 836 michezo ambayo imetoa nyota wengi sana, wafuatao ni nyota kumi na moja bora walioacha alama katika michuano hii.


1:LEV YASHIN : Kuna wakati nilitamani kumshuhudia Manuel Neur akishinda Ballon D’Or, lakini matamanio yangu yalikuja wakati mbaya, wakati ambao Cristiano Ronaldo na Messi wamezaliwa, ni bahati kubwa sana kushuhudia golikipa akibeba Ballon D’or, mwaka 1963 mababu zetu walimshuhudia Lev Yashin (Black Spider) akibeba Ballon D’or, huyu ndiye mfalme wa penalti, aliwahi kuchomoa michomo 150 ya penalti na kuwa na clean sheets 270.


2:Ushawahi kujiuliza ni beki gani namba mbili aliyewahi kutokea dunia akiwa amekamilika anapoenda kushambulia na kuzuia? Hapana shaka CAFU ni jina ambalo unaweza kulitaja, mshindi wa kombe la dunia 1994, 2002 na ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi za timu ya Taifa ya Brazil mechi 1994.


3:Hapana shaka historia itamkumbuka gwiji wa Brazil, PELE kipaji ambacho kiliwahi kutokea na inasemekana hakitokuja kutokea, ushawahi kujiuliza ni beki gani kisiki ambaye Pele anamkubali? Shughuli ya BOBBY MOORE ilikuwa shughuli pevu , nahodha wa Westham kwa miaka 10 na alikuwa nahodha wa England kipindi inashinda kombe la dunia 1966 na Pele anakiri huyu ndiye beki bora imara aliyewahi kukutana naye.


4:Maisha yako uliyaanzia wapi? Na utayamalizia wapi? Wengine maisha yao huanzia sehemu moja na kuyamalizia sehemu hiyo hiyo, FRANCO BARESI , Italy inamtambua kama beki wa kati bora kuwahi kutokea kwenye ardhi yao na alishinda kombe la dunia 1982. Maisha yake aliyaanzia Ac Milan na kuyamalizia Ac Milan.


5:Sir Alex Ferguson aliwahi kukiri kuwa PAOLO MALDINI ndiye mchezaji wa kipekee katika kizazi chake, kacheza kwa miaka 14 katika timu ya taifa na akiwa nahodha katika mechi 74 na akiwa amecheza michezo mingi kuzidi mchezaji yoyote kwenye timu ya taifa , michezo 126.


6:FRANZ BECKENBAUER. Ndiye mchezaji mwenye kipaji kikubwa kuwahi kutokea katika ardhi ya ujerumani. Alianza maisha yake ya soka kama kiungo wa kati na akawa beki imara wa kati (sweeper) na ndiye Mjerumani pekee aliyewahi kushinda kombe la dunia akiwa mchezaji na akiwa kocha (1974 na 1990).


7:Alama ya total football iliwekwa na JOHAN CRUFF, Genius wa mpira na mshindi wa ballon D,or mara tatu (1971,1973 na 1974).


8:Inawezekana ZINEDINE ZIDANE akawa mchezaji mwenye kipaji kikubwa cha sanaa ya mpira,lakini kwenye nafasi hii itabidi ampishe Michel Platin fundi pekee wa kucheza mipira iliyokufa kuwahi kutokea katika michuao hii.


9:DIEGO MARADONA, mchezaji pekee aliyeshinda Golden Ball mara mbili katika michuano ya kombe la dunia la chini U-20 na michuano ya Kombe la dunia. Mshindi wa kombe la dunia 1979 na mwaka 1986, mwaka ambao alifanikiwa kufunga magoli mawili, goli la mkono wa Mungu na goli la karne dhidi ya England.


10:Ukimtaja Messi lazima taswira ya Cristiano Ronaldo ije, hata nilipomtaja Maradona bila shaka picha ya PELE ilikuwa kichwani mwako. Mchezaji wa ajabu kuwahi kutokea duniani, aliyefunga hat tricks 90 katika maisha yake hapana shaka huyu ndiye mfungaji hatari wa wakati wote.


11:Ferenc Puskas, dunia imeshuhudia warembo wazuri sana lakini dunia ya mpira imeshuhudia wafungaji wengi wazuri lakini Ferenc Puskas anabaki kuwa mfungaji mzuri zaidi kwenye dunia hii ya mpira.


Sambaza....