Kipi kilichosababisha Manchester United washindwe?
Usiku wa kuamkia leo Manchester United walienda katika uwanja wa Wembley kama wageni wa Tottenham Hotspurs.
Uwanja ambao walikuwa hawajawahi kufungwa tangu mwaka 2011 ambapo walifungwa na Barcelona 3-1 katika fainali ya ligi ya mabingwa.
Baada ya hapa walishinda mechi 6 huku kila mechi wakifunga goli mbili, walikuwa na rekodi ya kuvutia kwenye uwanja wa Wembley lakini Jose Mourinho alikuwa na rekodi mbaya dhidi ya Mauricio Pochettinho. Mauricio Pochettinho kabla ya mechi ya jana alikuwa hajafungwa mechi tatu alizocheza nyumbani dhidi ya Jose Mourinho.
Kipi kikubwa kilichompa nguvu jana Mauricio Pochettinho?
Timu yake kucheza kwa ushirikiano ndicho kilikuwa kitu kikubwa kwa Tottenham Hotspurs.
Timu zote zilikuwa zinacheza mfumo wa 4-2-3-1 , mfumo huu ulionekana kuwa na faida kwa Hotspurs kwa kiasi kikubwa kuliko kwa Manchester United, kwa sababu Tottenham Hotspurs walikuwa na viungo wawili ambao kiasi ni wazuri sana kukaba, Eric Dier na Dembele, kumweka Dembele kwenye hii mechi kilikuwa na faida kubwa sana kwa sababu alikuwa na uwezo wa kushuka chini kuchukua mipira na kupanda nayo juu. Kitu ambacho Paul Pogba hakufanikiwa kukifanya, mara nyingi alishindwa kumsaidia Nemanja Matic katika majukumu yake ya kukaba hivo kumfanya Nemanja Matic kuwa peke yake na kuelemewa kwa kiasi kikubwa. Tofauti na kwa upande wa Eric Dier ambako alikuwa na usaidizi mkubwa wa Dembele.
Pili, wachezaji watatu wa Tottenham Hotspurs ambao walikuwa wanacheza nyuma ya Harry Kane ambao ni Son, Delle Ali pamoja na Erricksen walikuwa wanashuka katikati mwa uwanja kuongeza idadi ya viungo katikati ya uwanja.
Kuna wakati Manchester United ilipokuwa na mpira eneo la katikati mwa uwanja lilikuwa na idadi isiyokuwa na uwiano sawa kati ya wachezaji wa Tottenham Hotspurs. Mfano mara nyingi ilikuwa 2 v 4 au 3 v 5 yani wachezaji wawili wa Manchester United dhidi ya wachezaji wanne wa Spurs , au wachezaji watatu wa Mnachester United dhidi ya wachezaji watano wa spurs.
Hiki kitu hakikuleta uwiano mzuri eneo la katikati mwa uwanja hivo kuonekana Manchester United kuzidiwa kwa kiasi kikubwa eneo lile.
Ni kweli Manchester United bila Pogba huyumba?
Hapana shaka hili swali lina ukweli mkubwa ndani yake, kwa sababu Paul Pogba hupenda kukaa na mpira pamoja na kutengeneza nafasi. Jana Manchester United ilikuwa timu ambayo haikutengeneza nafasi kwa sababu Paul Pogba hakucheza vizuri.
Luke Shaw au Ashley Young?
Baada ya goli la kwanza kufungwa, Manchester United walijaribu kutumia upande wa kushoto kushambulia. Young alijaribu kupiga krosi, lakini kila kina Trippier walipokuwa wanashambulia kupitia kushoto Young hakuwa dhabiti kwenye jukumu la kujilinda.
Kuna haja ya Luke Shaw kuanza , na kama Luke Shaw haaminiki, kwenye dirisha la majira ya joto la usajili lijalo mkataɓa wa Luke Shaw unamalizika , hivo ni wakati mzuri wa Manchester United kuamua kubaki naye au hapana.
Hata kama wakibaki naye, kuna haja kubwa ya kusajili beki mwingine wa kushoto ambaye atasaidizana na Shaw kwa sababu Shaw hukubwa na majeraha ya mara kwa mara.
Kuna haja ya kuendelea kumwamini Jesse Lingard kama namba kumi wa Manchester United?
Hapana, Manchester United ni timu kubwa ambayo inahitaji wachezaji wengi wa kiwango kikubwa ndani ya kikosi ili kushindania makombe makubwa.
Moja ya sehemu ambayo Manchester United wanatakiwa kufanya marekebisho kwenye usajili ujao ni wao kusajili namba kumi bora ndani ya kikosi. Henrink ameshaondoka, Mesut Ozil kasaini mkataba mpya jana na Arsenal hivo tumaini kubwa lililobaki kwao ni kwa Paolo Dyabala wa Juventus.
Mwisho: Jana Tottenham Hotspurs ƙkilistahili kushinda kwa sababu walitawala mchezo , goli la kwanza lilionesha kuwachanganya mapema Manchester United kwa sababu hawakutegemea kukutana na mazingira kama yale