Sambaza....

Nakumbuka sana hisia nilizokuwa nazo, hisia ambazo zilinifanya nimwandikie makala ya utambulisho Shiza Ramadhani Kichuya.

Kipindi hicho ndiyo anaingia mjini. Ndiyo anakanyanga ardhi adhimu, ardhi ambayo Watanzania wengi hutamani kuikanyaga.

Ardhi ambayo hata ukiiacha na kwenda kukanyaga ardhi inayoitwa mkoani kila mmoja atatamani hata kuongea na wewe tu.

Lazima ubebe kijiji, kijiji ambacho kitakuwa na tamaa ya kukuona, kuongea na wewe, kukushika hata mkono , kisa tu umetoka Dar.

Dar es Salaam mji wa kibiashara, mji ambao kila aina ya biashara unayoifahamu hapa ndipo kitovu chake. Kwa kifupi kitovu cha biashara hapa Tanzania ni Dar es Salaam.

Ndiyo mji ambao ulimpokea Shiza Ramadhani Kichuya wakati anatoka kwao Morogoro, ndiyo mji ambao ulimuuza sana Shiza Ramadhani Kichuya.

Kila jicho lilianza kufurahia kipaji cha mguu wake wa kulia, polepole akaanza kujipenyeza katikati ya mioyo ya mashabiki wa Simba.

Walianza kumhusudu sana, palepale na mimi nikatumia nafasi yangu ya kumkaribisha Shiza Ramadhani Kichuya. Naikumbuka sana makala yangu ya “Shiza Karibu kwenye kioo cha kinyozi”

Kioo ambacho kinyozi hutumia muda mchache kuwa na wewe, atatumia muda mchache kuongea na wewe. Atacheka na wewe, atafurahia na wewe.

Na tena atakuongezea tabasamu pana kipindi anapokunyoa huku akiwa anakusifia kuwa una muonekano mzuri, maneno ambayo utayapokea kwa tabasamu pia.

Kwa kifupi kwenye kioo hiki kitu kinachowaunganisha mnyoaji na yule anayenyolewa ni kitu kimoja tu tabasamu la muda mfupi.

Baada ya hapo thamani ya anayenyolewa huisha, na mnyoaji hufikiria mtu mwingine tofauti tena na siyo wewe.

Thamani ya Shiza Ramadhani Kichuya ilikuwa kipindi kile yuko Simba. Kipindi ambacho alikuwa na uwezo wa kupiga kona na kuingia moja kwa moja golini.

Kipindi ambacho Shiza Ramadhani Kichuya alikuwa anatengeneza tabasamu la mashabiki wa Simba kila alipokuwa anaifunga Yanga.

Ndicho kipindi ambacho tabasamu la shabiki wa Simba lilikuwa linaungana na tabasamu la Shiza Ramadhani Kichuya.

Tabasamu ambalo kwa sasa haliwaunganishi tena. Hawako pamoja tena. Shabiki wa Simba hamkumbuki tena Shiza Ramadhani Kichuya, shabiki kwa sasa anamuwaza Deo Kanda na Francis Kahata.

Hana muda wa kumuwaza tena Shiza Ramadhani Kichuya kwa sababu tu tayari ashalipia hela ya kunyolea. Hana thamani tena kwenye macho yao, aliye na thamani ni yule ambaye yuko mkononi mwake.

Inawezekana kabisa kwa sasa Shiza Ramadhani Kichuya anaiwaza sana Simba, anaikumbuka sana Simba lakini kwa asilimia chache Simba inaweza ikawa haimkumbuki yeye.

Yuko sehemu mbaya, sehemu ambayo awali hakuwepo. Sehemu ambayo hakuzoea tena kuishi. Shiza Ramadhani Kichuya alikuwa anaishi maisha mazuri.

Maisha yenye raha, maisha ambayo yalikuwa yamejaa upendo mkubwa ndani yake. Kwa sasa upendo haupo tena. Hapendwi tena na kujaliwa kama awali.

Inawezekana kuna sehemu alikosea katika hatua zake za maisha ya mpira, inawezekana kabisa kuna uzembe ambao aliuonesha.

Uzembe ambao mpaka sasa umemfanya asiwe na timu na yuko Morogoro tu. Inauma sana kuona kipaji cha Shiza Ramadhani Kichuya kikiwa kinakaa muda mrefu bila kucheza.

Inauma sana kuona kipaji chake kikiwa hakina msaada kwenye timu ya taifa. Hiki ndicho kipaji ambacho kilifaa kuwa karibu na mafanikio ya Mbwana Ally Samatta sema kimekosa neno jitihada kwenye maisha yake.

Jitihada ambayo ingemjengea paradiso yake ya mpira, leo hii hayupo huko. Yuko hospitali, anaumwa sana na tusipoangalia tutampoteza siku yoyote.

Uwezekano wa kumponesha upo kabisa, bado taifa linauhitaji sana mguu wake wa kushoto. Mguu wake una thamani kubwa sana kwenye maisha yetu ya mpira.

Mguu wake wa kushoto unauwezo wa kutupeleka Qatar. Mguu wake wa kushoto ni VISA tosha ya kutupeleka popote tunapohitaji kwenda lakini umekosa jitihada tu.

Umelemaaa sana. Haujachangamka hata kidogo. Umekuwa mguu mzito sana, hautaki hata kukimbia kwa sasa, hata kutembea unalazimishwa kutembea huu mguu.

Tunauhitaji sana mguu wa Shiza Ramadhani Kichuya, tunao uwezo wa kuukoa. Sawa kwa sasa uko ICU ya mpira wa miguu lakini tunauwezo wa kufanya changizo na yeye kwenda India ya mpira wa miguu kwa matibabu.

Sambaza....