Ushawahi kumfuatilia Shiza Kichuya akiwa anacheza dhidi ya Simba?, ushawahi kushuhudia ile hali kubwa ambayo hujaa ndani yake?
Upiganaji wake ushawahi kuuona?, huwa hachoki , muda mwingi huwa anatamani awe na mpira kwenye miguu yake.
Njaa huwa karibu naye kila anapokuwa anacheza na Yanga. Hii ndiyo mechi ambayo kipaji halisi cha Shiza Kichuya huwa kinaonekana.
Unaweza kuwashuhudia wachezaji wa Simba wamepoteana sana kwenye mechi hii lakini siyo kwa Shiza Kichuya.
Huyu huwa anabaki kuwa hai peke yake hata kama wenzake wakiwa hoi taabani kuelekea sekunde za kifo. Huwa hafai mapema kwenye mechi hii.
Muda wote pumzi yake huwa ya moto sana. Kama wakala hutakiwi kushawishika kabisa kumsajili kwenye mechi hii.
Mechi hii anaweza kukuonesha kiwango kikubwa sana lakini kwenye mechi zingine akakusikitisha sana na unaweza ukamtukana kila aina ya matusi.
Huyu ndiye Shiza Kichuya, muuaji wa Yanga kwa mechi za hivi karibuni. Na inasemekana yeye kazaliwa kwa ajili ya kucheza zaidi kwenye mechi hii.
Mechi ambayo hubeba hisia kubwa nchini. Ni mechi ambayo husimamisha nchi kwa dakika 90. Kila jicho huwa Dar es Salaam.
Kila sikio hutamani kusikia kinachotokea pale kwenye uwanja wa Taifa. Hii ni kwa sababu timu hizi zimezigawa nchi katikati.
Kuna upande wa jangwani na kuna upande wa msimbazi. Huu ndiyo mgawanyo halisi. Ndiyo maana kuna wachezaji huwa wanatamani kuonekana nyota kwenye michezo kama hii.
Hawa ni kina Shiza Kichuya. Wao hutamani sana kuonekana kama mashujaa na hutamani sana wasifiwe baada ya mechi.
Ndiyo maana hujitoa kwa kiasi kikubwa kwenye aina hii ya mechi. Kwa kifupi hii ni aina ya mechi za hawa watu.
Kuna kipindi hii damu alikuwa nayo pia Emmanuel Okwi. Naamini bado anayo, yeye pia huwa anacheza sana kwenye aina ya mechi hizi.
Huyu ni mchezaji wa mechi kubwa hasa hasa zile ambazo huwa zinachezwa kwenye uwanja wa Taifa. Uwanja ambao ulitengenezwa kwa ajili yake kabisa.
Na mechi ya kesho inapigwa kwenye uwanja huo. Na mechi hiyo ni mechi kubwa kama mechi kubwa zingine ambazo Emmanuel Okwi huwa anang’ara.
Pamoja na kwamba Yanga huwa wanamhofia sana Shiza Kichuya, lakini ni ukweli uliowazi kuwa muuaji mwingine wa Yanga ni Emmanuel Okwi.
Amekuwa na tabia ya kuwaadhibu Yanga kila anapokutana nao. Inawezekana kabisa wanaweza wakawa wamepumua kuondoka kwa Shiza Kichuya , lakini kazi inabaki kwa Emmanuel Okwi.
Na kitu kibaya zaidi Emmanuel Okwi kwa sasa yupo kwenye kiwango kikubwa sana. Kiwango ambacho kinachagizwa na ukomavu wake aliofikia muda huu.
Muda huu Emmanuel Okwi kakomaa sana kuliko misimu ya nyuma. Anajua kufanya maamuzi ambayo ni bora kwake na timu yake kwa ujumla.
Miguu yake haina vitu vingi kama zamani, kwa sasa anawaza kufunga na kutoa pasi za mwisho zenye kusababisha goli.
Hana ubinafsi wa kitoto kama zamani, anaiwaza timu sana kwa sasa . Kwake yeye timu ndicho kitu cha kwanza kinachokuja katika akili yake.
Ndiyo maana huwa anatengeneza nafasi nyingi kwa ajili ya timu kushinda. Kitu ambacho kinaashiria ukomavu katika ajili ya Emmanuel Okwi.
Pamoja na kwamba Emmanuel Okwi amekuwa akitengeneza nafasi nyingi kwa ajili ya timu yake , pia amekuwa mfungaji mzuri sana.
Anafunga katika eneo lolote lile, anafunga kwa mashuti ya mbali, kwa kupiga mipira iliyokufa na hata ndani ya eneo kumi na nane.
Ukiachana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi nyingi za magoli pamoja na uwezo wake wa kufunga. Kuna kitu kingine cha ziada kimezaliwa kwa Emmanuel Okwi.
Uongozi! , Emmanuel Okwi amekuwa kiongozi mzuri ndani ya kikosi cha Simba. Pamoja na kwamba siyo nahodha mkuu lakini amekuwa ni kiongozi ndani ya uwanja.
Hii kuna faida kubwa sana kwake na kwa timu, kwa sababu unapokuwa kiongozi ndani ya timu lazima ufanye kitu ambacho wengi watakuona kama mfano mkubwa.
Emmanuel Okwi yuko hivo kwa sasa, anajiona kama kiongozi mkuu ndani ya timu ya Simba. Jambo ambalo ni zuri sana.
Ndiyo maana anajituma sana kwa kuonesha kuwa yeye ni mfano mzuri kwa wengine. Kiasi kwamba hata kama akimkumbusha majukumu mchezaji mwingine ni virahisi kwa huyo mchezaji kuyafanya majukumu yake kwa sababu tu kamuona Emmanuel Okwi anajituma ndani ya uwanja.