Baada ya Shiza Ramadhani Kichuya kurejea nyumbani akitokea Misri maneno mengi yamekuwa yakisemwa kuhusiana na sababu ya yeye kurudi tena sehemu ambayo inaonekana kama ni hatua za kurudi nyuma.
Watu wengi walikuwa wanategemea Shiza Ramadhani Kichuya angeendelea kucheza soka la kulipwa kwa manufaa yake binafsi na kwa manufaa ya mpira wetu .
Mpira wetu unahitaji wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa katika nchi ambazo zimeendelea kisoka. Jambo hili la Shiza kichuya kurudi Simba limemshangaza mchezaji wa zamani wa Simba na timu ya Taifa , Mtemi Ramadhani.
Akizungumza na kituo cha radio hapa nchini cha Wasafi Fm , Mtemi Ramadhani alidai kuwa Shiza Ramadhani Kichuya hakutakiwa arudi nyumbani alitakiwa asonge mbele .
“Mimi nilitegemea yeye kuendelea kusonga mbele zaidi , kurudi Simba kwangu Mimi naona kama amerudi nyuma kwenye hatua zake za maendeleo”- alisema mchezaji huyo wa zamani wa Simba .
Alipoulizwa kuhusu kama Shiza Ramadhani Kichuya ameimarika kiuchezaji tangu arudi Simba kutoka na mechi moja ambayo amecheza , mchezaji huyo wa zamani wa Simba amedai kuwa kashuka sana.
“Kuna muda ukiwaona kina Mbwana Samatta wamerudi unaona mabadiliko makubwa katika uchezaji wao , Lakini kwa Shiza Ramadhani Kichuya imekuwa tofauti kabisa kwa sababu hajaimarika sana”- alizidi kusema mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Taifa.
Kuhusu nafasi yake katika kikosi cha timu ya Simba , Mtemi Ramadhani amedai kuwa nafasi ya Shiza Ramadhani Kichuya ni finyu sana katika kikosi hicho na ataendelea kukaa Benchi.
“Nafasi yake ni finyu Sana kwa sababu eneo ambalo anacheza ni eneo ambalo linawachezaji wengi wazuri . Kwa hiyo ni ngumu kwake yeye kupata nafasi ya moja kwa moja . Kwa wachezaji waliopo atakaa sana benchi”- alimalizia kusema Mtemi Ramadhani.