Yanga na Rivers United. Simba na Waydad Casablanca. Mechi ya Simba na Waydad imekuwa mjadala mkubwa kuliko mechi ya Yanga na Rivers United. Mechi ya Yanga inazungumzwa sehemu ndogo, sehemu kubwa inazungumzwa mechi ya Simba.
Hii inashusha Joto la wachezaji wa Yanga, hawajioni kama wana kazi kubwa ya kufanya. Nawafahamu wachezaji walivyo. Wachezaji wana mitandao ya kijamii, wanaona kinachoandikwa juu ya mechi yao na mechi ya Simba.
Mastaa wa Yanga sujui kama wanajiona wana kazi kubwa ya kufanya. Wengi wetu tumewabeza Rivers na tumewapitisha Yanga hatua ya nusu fainali. Tunaamini mechi iko kwa Simba na Waydad, kule kwa Yanga kuna kwenda kukamilisha ratiba. Hata mioyo ya mashabiki wa Simba na Yanga iko tofauti.
Yanga wanaamini wana mechi rahisi, Simba wanaamini wana mechi ngumu ( Japo ukweli ndiyo huu). Anachojisikia Tshabalala ni tofauti na anachojisikia Lomalisa katika nyakati hizi wakikaa mbele ya TV kutazama mikanda ya wapinzani wao.
Lakini tunapaswa kujiuliza kati yetu nani kawaona Rivers hivi karibuni? Hilo linabaki kuwa swali gumu. Wengi tunawahukumu Rivers kwa tulivyowaona mara ya mwisho walivyocheza na Yanga. Kisha tunapima kuimarika kwa Yanga. Tukitoka hapo moja kwa moja tunaona Rivers kashatolewa na Yanga kasonga mbele.
Naomba nirudie, kati yetu nani amewaona Rivers hivi karibuni? Hilo linabakia kuwa swali gumu zaidi katika nyakati hizi.